Klabu ya Singida Fountain Gate inayoshiriki Ligi kuu kandanda Tanzania Bara imemtangaza Heron Ricardo Ferreira (65) Raia wa Brazil kuwa kocha mpya wa kikosi hicho akichukua nafasi ya Ernest middendorp aliyeondoka kikosini hapo wiki chache zilizopita. Ricardo atakuwa na wasaidizi wake ndani ya kikosi hicho, huyu anakuwa kocha wa tatu kukiongoza kikosi cha Singida Fountain Gate msimu huu.
Ricardo anaudhoefu wa kutosha wa kufundisha Barani Afrika akipita kwenye Klabu kadhaa ikiwemo Al Hilal ya Sudan aliyodumu nayo kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2005-2008 akiipatia ubingwa wa Ligi kuu nchini Sudan mara tatu kuanzia mwaka 2005/05, 2005/06, 2006/07 na kufanikiwa kuifikisha klabu hiyo nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2006/07.
Ricardo aliwahi kupita kwenye klabu ya Ismaily ya Misri msimu wa 2020/21 na kuiongoza kwenye michezo mitatu pekeee ya Ligi na klabu hiyo ikaamua kumfuta kazi.
Msimu wa 2022/23 Ricardo alikuwa akiinoa Al Merrikh na alifanikiwa kuifikisha hatua ya makungi ya Ligi ya mabingwa Barani Afrika kabla hajatimkia Singida Fountain Gate.
Ricardo amewahi kupata tuzo mbalimbali zikiwemo Kocha bora wa Ligi ya Sudan mwaka 2012,2007, 2006 na 2005. Alipata tuzo ya kocha bora wa pili barani Afrika msimu wa 2007/08. Tuzo ya kocha bora wa pili nchini Misri msimu wa 2008/09. Kocha bora nchini Parana msimu wa 1996-94.
Baada ya kutambulishwa kuwa kocha mpya wa kikosi cha Singida Fountain Gate amesema analijua soka la Tanzania kwani kuna kipindi aliwahi kuja nchini kucheza dhidi ya klabu moja wapo kati ya Simba na Yanga msimu wa 2006/07 kwenye Ligi ya mabingwa Barani Afrika na waliweka kambi visiwani Zanzibar.
Baada ya kutambulishwa ndani ya kikosi cha walima Alizeti kocha Ricardo akasema amekuja kutoa ushindani wa kutosha kwa timu za Simba na Yanga ambazo zinaonekana kupokezana mara kwa mara kwenye kubeba ubingwa wa Ligi kuu Tanzania Bara na lengo lake ni kutengeneza timu ya ushindani.
Ninaudhoefu wa kutosha na soka la Afrika, matokeo yangu mazuri wakati nikiwa Sudan ilikuwa ni kufika nusu fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika nikiwa na Al Hilal, mimi ni mtu wa kutoa ushindani, na naona nina nafasi nzuri ya kufanya kitu tofauti hapa Singida, ukiangalia orodha ya ubingwa wa Ligi kuu utaziona Simba na Yanga zinapokezana, nimekuja hapa kujaribu kubadili hili, siwaahidi kubeba ubingwa lakini nitatengeneza timu nzuri na ya ushindani kupambana kwenye kiwango sawa, mpira sio maajabu mpira ni muda wa kutengeneza timu.
Heron Ferreire kocha mkuu wa Singida Fountain Gate