Kocha mkuu wa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania Adel Amrouche baada ya mchezo wa jana dhidi ya Sudan uliomalizika kwa sare ya kufungana goli 1-1 huko Saudi Arabia, alisema mchezo ulikuwa mzuri na ni lazima ufike wakati timu kubwa Tanzania ziwape nafasi magolikipa wazawa na ziache kutumia magolikipa wa kigeni. Adel aliyasema hayo baada ya kuonekana makosa mengi kwenye eneo la golikipa kitu ambacho kilipelekea timu yake kufungwa goli la mapema jambo ambalo aliamini ni makosa ya golikipa.
Kwenye timu ya Taifa hatuwaendelezi wachezaji bali kwenye klabu, kuhusu stori ya golikipa wetu ni kwamba Tanzania lazima wabadilike kuwa sio lazima magolikipa wa kigeni wacheze kwenye klabu kubwa, tunahitaji magolikipa wetu wacheze, lazima tuwape muda wa kucheza, kila mtu ameona leo sio rahisi kama tusingewapa magolikipa wetu nafasi ya kucheza leo, tuna magolikipa lakini bila ushindani si kitu, sasa hivi tunahangaika na mambo mengi ikiwemo siasa hizi za kuita wachezaji, najua shirikisho linalifanyia kazi, hii ni Tanzania tunacheza kwaajili ya Taifa na sio klabu.
Kocha mkuu Taifa Stars Adel Amrouch baada ya mchezo dhidi ya Sudan.
Kocha Adel amesema pia kuwa timu ta Taifa sio sehemu ya kuendeleza wachezaji bali wachezaji wanapaswa kuendelezwa na klabu zao, na pia ataita wachezaji kulingana na ubora wanaouonyesha kwenye klabu zao na sio kuangalia majina ya wachezaji, kwa wale watakaoshindwa kuonyesha uwezo kwenye klabu zao basi hawatapata nafasi.
Kwa upande wa nahodha wa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania Mbwana Ally Samatta amesema michezo ya kirafiki wanayocheza ni kipimo kizuri kuelekea katika michezo ya mashindano na mwalimu atatoa tathimini yake kuhusu kile alichokiona kwenye mchezo dhidi ya Sudan.
Kwaupande wa kocha mkuu wa kikosi cha Sudan James Appiah amesema ni kwa mara ya kwanza ameishuhudia tiu yake ya Sudan ikicheza na imecheza vizuri.
Tanzania imecheza vizuri hasa kipindi cha kwanza, kabla ya kipindi cha pili Sudan kuingia mchezoni, hii ni mara yangu ya kwanza kuishuhudia Sudan ikicheza nadhani wamefanya vizuri na wanaweza kufanya vizuri zaidi ya hapa, Tanzania sio nchi ndogo kwenye mpira, changamoto yao ni eneo la umaliziaji lakini kiufundi wanacheza vizuri.
Kocha wa Sudan James Appiah.
Goli kwa upande wa Tanzania lilifungwa na Sospeter Bajana dakika ya 40 na kwa upande wa Sudan lilifungwa na Musab Ahmed dakika ya 7 ya mchezo. Tanzania ipo kwenye maandalizi ya michezo ya kufuzu fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco inayotarajiwa kupigwa mwezi November.