Gwiji wa soka wa zamani wa Manchester United na Uingereza, Sir Bobby Charlton amefariki dunia hii leo akiwa amezungukwa na familia yake mapema asubuhi ya leo akiwa na umri wa miaka 86 huku sababu za kifo chake kikielezwa kuwa ni DEMENTIA(SHIDA YA AKILI).
Sir Bobby Charlton enzi za uhai wake alikuwa ni moja wa mashujaa wa Uingereza baada ya kuiongoza timu ya taifa lake kutwaa Ubingwa wa kombe la dunia mwaka 1966. Kufuatia kifo chake, ni Sir Geoff Hurst(alifunga magoli matatu kwenye ushindi wa 4-2 dhidi ya Ujerumani Magharibi) pekee ndiye anayebaki kuwa hai kutoka kwenye kikosi kile kilichotwaa ubingwa wa dunia. Anafariki akiwa amecheza mechi 758 huku mechi 106 akiitumikia timu yake ya taifa.
Upande wa klabu anakumbukwa kama moja ya wachezaji hodari kuwahi kutokea kwenye historia ya Klabu. Sanamu lake limewekwa sambamba na nyota wengine, George Best na Dennis Law(pekee aliye hai kwenye sanamu hilo). Akicheza mechi 758 na kufunga mabao 249 kwa United kati ya msimu 1956-1973. Itakumbukwa pia ajali mbaya ya Munich 1958 iliyoua wachezaji wenzake takribani 8 wa kikosi cha kwanza, yeye alikuwa ni mmoja wa wahanga waliotoka hai, na kabla ya kifo chake ndiyo mchezaji pekee aliyebaki hai. Alifanikiwa pia kuipa United kombe la ligi ya mabingwa mwaka 1966.
Aligundulika na ugonjwa huo wa Shida ya akili Novemba, 2020 ikiwa miezi minne tu tangu kaka yake Jack Charlton ambaye pia ni miongoni mwa mashujaa wa kombe la dunia 1966, afariki akiwa na miaka 85 na alianza kujitenga na jamii.
Sir Bobby Charlton amefariki siku 10 tu tangu asherehekee siku yake ya kuzaliwa. Alizaliwa tarehe 11/10/1937 na ameacha mke, Lady Norma na watoto wakiwemo Suzanne na Andrea ambao walikuwa naye mpaka umauti unammfika.
Manchester United wanatarajiwa kuvaa vitambaa vyeusi leo kwenye mchezo wao dhidi ya Sheffield United hapo baadae, Saa 4 usiku kwenye mchezo wa ligi kuu. Wao waliandika kwenye ukurasa wao wa Instagram, “MANENO HAYATOSHI KUELEZEA”
Mungu Ailaze Roho ya Marehemu SIR BOBBY CHARLTON MAHALA PEMA PEPONI