Connect with us

AFL

TP MAZEMBE YATAKATA KWA MKAPA

Ikionekana kama vile wamezidiwa na wapinzani wao Esperance, TP Mazembe walikuwa na dakika 10 za moto sana wakishambuliwa mfululizo huku bado pakionekana hakuna utulivu kwenye safu yao ya ulinzi na kummpa wakati mgumu golikipa wao Baggio Saidi kudhibiti heka heka kadhaa langoni mwake.

Dakika ya 11 ya mchezo, kibao kiligeuka, TP Mazembe wakapata goli la kushtukiza kupitia kwa Mmali, Cheikh Fofana akimalizia kwa kichwa krosi safi kutoka kwa Phillipe Kinzumbi aliyepokea pasi fupi kutoka kwenye pigo la kona.

Mazembe wakauchukua mchezo kuanzia hapa, huku Fofana, KInzumbi na Hainikoye wakilisakama goli la Esperance na kuwapa wakati mgumu walinzi wao. Utasifu uhodari wa golikipa Amannallah Memmich aliyekuwa mtulivu kuipoza timu, Mazembe walikuwa wanajiskia kweli wapo nyumbani. Wakishangiliwa na mashabiki lukuki waliojitokeza uwanja wa Mkapa hii leo.

Esperance nao hawakuwa wanyonge walijaribu kusukuma mashambulizi kupitia upande wa kulia wa Mazembe, mashariki ya uwanja kupitia kwa Oussama Bouguerra ambaye alikuwa akishirikiana vizuri na Kebba Sowe, lakini bado mashambulizi yao hayakuzaa matunda. Mpaka mapumziko, TP Mazembe alikuwa akiongoza kwa 1-0.

Mwalimu Lamine Ndiaye alianza kipindi cha pili na mabadiliko, akimmpumzisha Ousseini Badamassi na kumuingiza Augustine Oladapo. Dakika ya 49 tu ya mchezo, Hainikoye alipokea pasi kutoka kwa Kinzumbi nje kidogo ya 18 na kuachia shuti kali lililopaa juu kidogo ya lango la Esperance.

Dakika ya 60 ya mchezo, Esperance wakafanya mabadiliko na wao kwa kummtoa Kemba Sowe na Kumuingiza Mbrazili Rodrigues Silva. Akitoka pia Mootez Zaddem na nafasi yake kuchukuliwa na Mbrazili  mwingine Yan Sasse. Mbadiliko ya kiufundi ya kuongeza kasi ya mashambulizi kutafuta goli la kusawazisha.

Haikuchukua muda muunganiko wa mabadiliko haya kufanya kazi, dakika 2 tu baadae, wabrazili hawa walipeana pasi ndani ya eneo la Mazembe na Yan Sasse kutumbukiza kimiani goli la kusawazisha lakini likakataliwa na VAR akimmshauri muamuzi wa kati kuwa kabla Rodrigues hajapiga pasi kwa Yan Sasse alikuwa kwenye nafasi ya kuotea. Ikaendelea kusalia 1-0 kwa Mazembe mpaka dakika ya 64.

Dakika ya 68, Mazembe walifanya mabadiliko mengine, Boubacar Hainikoye alimmpisha Alex Ngonga.

Phillipe Kinzumbi aliwakumbusha Esperance kuwa yupo na ni mchezaji wa kuchungwa sana baada ya kuachia shuti kali dakika ya 75 akiwa ameachwa huru sana  ikimmlazimu Mammiche kujikunjua na kufanya pengine uokoaji bora wa mechi mapaka dakika hizo za mchezo.

Dakika ya 82 anaingia  Joel Beya nafasi ya Cheikh Fofana upande wa Mazembe na Dakika ya 85 Esperance nao wakafanya mabadiliko kwa kuwatoa Zakaria El Ayeb, Mohamed Ben Ali  na Oussama Bouguerra nafasi zao kuchuliwa na Mohamed Amin Tougai, Ghaith Ouahabi na Mohamed Ali Ben Hammouda, wakati huo huo Mazembe wakamuingiza Zemanga Soze nafasi ya Glody Likonza.

Mazembe bado waliendelea kulisakama lango la Esperance kutafuta goli la 2 ili kujiwekea nafasi nzuri zaidi kwenye matokeo ya jumla kabla ya kwenda Tunis. Lakini mpaka mpira unamalizika, TP Mazembe walibaki na ushindi wa goli 1-0 kwenye mchezo uliokuwa na burudani ya aina yake.

Makala Nyingine

More in AFL