Connect with us

Azam FC

AZIZ KI AWAPAISHA WANANCHI KILELENI

Dabi ya Dar es Salaam inamalizika, Azam wanashindwa kufua dafu mbele ya Yanga kwa mara nyingine tena. Kwa mara ya 4 mfululizo, Azam anachapika na Azizi Ki anaibuka shujaa. Yanga anapaa hadi nafasi ya 1 ya Msimamo wa ligi kuu baada ya matokeo haya.

Azam waliuanza mchezo kwa kasi ya kushtukiza na dakika ya 2 tu ya mchezo walipata kona ilichongwa na Cheikh Sidibe lakini ikaondolewa na walinzi wa Yanga.

Dakika ya 4 ya mchezo, Pacome Zouzoua alimmtengea pasi Maxi Nzengeli aliyepiga mkwaju wa chini chini uliopita nje kidogo ya lango upande wa kulia wa Idrissu

Wakati mchezo ukibadilisha hatamu yake kwa Yanga kuuchukua mchezo, dakika ya 8, Nahodha Mwamnyeto alipiga pasi ndefu kwa Azizi Ki akiwa katika mazingira yaliyoonekana kuwa magumu, lakini akafanikiwa kummpita mlinzi wa Azam, Malickou Ndoye na kisha kwenye pembe ngumu akaupitisha mpira katikati ya miguu ya Idrissu Abdoulaye na mpira kujaa kimiani. 1-0 kwa Yanga.

Mpira uliongeza kasi baada ya hapa, ni kama Yanga walicharuka kutaka kupata na goli jingine mapema mapema, Azizi Ki, Pacome Zouzoua na Maxi walikuwa wakipishana vizuri lakini ulinzi wa Azam ulilazimika kuzidisha umakini.

Dakika ya 18, Azam walifanya shinikizo la kushtukiza na likalipa. Djibril Sylla alifanya mkimbio upande wake wa kulia, kisha kupeana pasi nzuri na Lusajo Mwaikenda(one-two), akajitengenezea nafasi na kupiga shuti la chini pembeni kabisa upande wa kushota wa Diarra ambaye alijinyoosha kujaribu kuokoa lakini hakufua dafu. Bonge la goli alifunga Sylla kufanya mzani kuwa sawa.

Mechi ilionekana kutulia baada ya hapo, kila timu ikijihami na kushambulia kwa kukushtukiza. Rapsha za hapa na pale hazikukosekana lakini dakika ya 34, Azizi Ki aliachia mkwaju kwa mguu wake wa kushoto lakini Idrissu alikuwa sambamba nalo, akiupaka mafuta. Kona iliyopatikana haikuzaa matunda.

Dakika 2 baadae, Bado bundi aliendelea kuzengea goli la Azam, safari hii Mudathir alipokea pasi nzuri kutoka katikati ya kiwanja akiwa peke yake na golikipa alipiga mpira uliommbabatiza Idrissu na mpira kwenda nje kuwa kona. Kwa mara nyingine tena, kona ikawa tasa.

Azam waliamua kufanya utulivu na kukaa na mpira walahu kupunguza kasi ya mashambulizi ya wapinzani wao, wakati huu Feisal Salum akitamba kwenye eneo la kiungo, alichezewa faulo kwenye eneo karibu na lango la Yanga. Mpira uliokufa ukichongwa na Cheikh Sidibe, ilimmlazimu Diarra afanye kazi ya ziada kuokoa mpira huo. Kona ya Sidibe pia haikuwa na faida kwa Azam. Dakika 45 zikamaliziika kwa sare ya 1-1.

Kipindi cha pili kilirejea kwa kasi ya kawaida, kila kitu kikifanyika kimmkakati na hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanywa na walimu wote wawili. Dakika ya 48 Pacome Zouzoua alipata nafasi lakini shuti lake lilibabatiza walinzi na kuwa kona.

Mchezo ukiwa unashika kasi taratibu kipindi hiki cha pili, shoka nalo halikuwa mbali. Zilitembea buti kadhaa bdani ya dakika 2, wahanga wa kadi za njano wakiwa ni Khalid Aucho aliyemmchezea faulo Feisal Salum dakika ya 55 na Sospeter Bajana aliyemmkwatua Mudathir Yahya dakika ya 57. Na mbona mpira ukaendelea kupigwa kwa kasi ile ile. Mpira ulichangamka sana mpaka dakika hizi.

Dakika ya 60, Azam walipatiwa mkwaju wa penati  baada ya Bakari Mwamnyeto kummfanyia madhambi Djibril Sillah ndani ya eneo la penati na Prince Dube hakufanya makosa na kuipatia Azam bao la pili la kuwapa uongozi. Bakari Mwamnyeto akionyeshwa kadi ya njano kwa madhambi hayo. 2-1 Azam.

Feisal Salum ni kama alikuwa na kisasi na waajiri wake wa zamani, akichanja mbuga upande wake wa kushoto akiwaacha chini Dickson Job lakini safari yake ikakatishwa na Mudathir Yahya karibu kabisa na eneo la Yanga. Mudathir alizawadiwa kadi ya njano kwa madhambi hayo. Mwalimu Gamondi alimmfanyia mabadiliko punde na kumuingiza Moloko.

Dakika ya 68, Stephane Aziz alidondoshwa karibu kabisa na eneo la Azam na Lusajo Mwaikenda na akaonyeshwa kadi ya njano. Faulo akiichonga kiustadi  yeye mwenyewe, mpira ukionekana kama hauna madhara, unammshinda Idrissu na mpira kutinga wavuni na Yanga kusawazisha.

Dakika ya 71, Stephane Azizi Ki tena, anawanyanyua Wananchi vitini kwa kupachika bao la 3 kwake na kwa timu yake, Hattrick. Anapokea pasi elekezi kutoka kwa Khalid Aucho na kumzungushia Idrissu pembeni mbali kabisa kuipa uongozi Yanga. Nyakati tamu sana kwake ilikuwa.

Azam wakafanya mabadiliko dakika ya 77 kwa kuwatoa Abdul Sopu na James Akaminko na kuwaingiza Kipre Jr. na Yannick Bangala. Yanga wanafanya mabadiliko ya kiufundi pia dakika ya 83 akitoka mshambuliaji Clement Mzize akaingia Kiungo Mkabaji Zawadi Mauya kubadili mfumo kuwa 4-3-3 Flat. Azam nao wakajibu kwa kummtoa Kiungo mkabaji Sospeter Bajana na kumuingiza kiungo mshambuliaji Iddy Nado huku Prince Dube akitoka kummpisha Idris Mbombo.

Dakika ya 89, Yanga wakafanya tena mabadiliko kwa kummpumzisha Aziz Kin a kuingia Hafiz Konkoni huku muamuzi wa akiba akionyesha dakika 4 za nyongeza.

Mwamuzi Ahmed Aragija, anapuliza kipyenga kumaliza mchezo. Yanga wanapata ushindi wa 3-2.

Makala Nyingine

More in Azam FC