Connect with us

Azam FC

YANGA YAISHIKA PABAYA AZAM

Mchezo dume kwa siku ya leo. Mchezo wa kimaamuzi kwa timu zote mbili kwenye harakati za kuwania nafasi za juu mapema kwenye msimamo wa ligi kuu ya NBC na bila shaka haijawahi kuwa mechi nyepesi wanapokutana wanaume hawa wawili, na mechi yao hii kubaatizwa DABI YA DAR ES SALAAM. Ama hakika inastahili.

Ni Sare 1 tu imepatikana katikati yao kwenye michezo 6 ya hivi karibuni na ni sare ya 2-2 kwenye uwanja wa Mkapa, msimu uliopita, michezo mingine yote iliwa kwenye faida ya Yanga. Yanga imewashika pabaya sana Azam.

Wote wametoka kushinda michezo yao ya mwisho ya ligi, Yanga akiifumua Geita Gold 3-0 kwenye Uwanja wa Shule ya Nyankumbu huku Azam wakipata ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Mbweha, Mangush ama Wagosi wa Kaya, Coastal Union kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani. Wote bado wana ari  nzuri kuelekea mchezo huu.

Yanga hutumia mfumo wa 4-2-3-1 hali kadhalika Azam, japo wao hutumia 4-4-2 pia kama mfumo mama. Kwenye michezo miwili ya mwisho ya Yanga, Mwalimu Gamondi alipanga vikosi viwili tofauti lakini hakubadili mfumo. Mwalimu Dabo kwa upande wake hakufanya mabadiliko makubwa sana kutoka kwenye kikosi kilichotoa suluhu ya 0-0 na Dodoma Jiji alipocheza dhidi ya Coastal Union japo alitumia 4-4-2 dhidi ya Dodoma na 4-2-3-1 dhidi ya Coastal Union.

Eneo la kiungo ndilo litakalokuwa jiko kuu la mchezo huu. Kuna namba nyingi sana za kuogopesha upande wa Yanga. Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua wana jumla ya mabao 5 kwenye michezo ya hivi karibuni. Pacome akitoka kufunga magoli mawili(2) kwenye michezo miwili mfululizo, dhidi ya Ihefu na Geita Gold. Ni eneo hili utammkuta mwanaume wa nyakati hizi kwa Yanga, Stephane Aziz Ki na kwa pamoja utatu huu unammlisha Kijana Clement Mzize akicheza kama Mshambuliaji pekee, lakini  namna wanavyopishana kwenye eneo la kushambulia ni mauaji. Aucho na Mudathir ni wasindikizaji wa kuhahikisha haya yote yanafanyika pasi na shaka.

Azam sio wanyonge pia kwenye eneo hili. Magoli 10 kwenye mechi 5 inakupa wastani wa goli 2 kila mechi, sio haba kabisa. Feisal Salum amekuwa kwenye moyo wa haya yote mara nyingi akicheza nyuma ya mshambuliaji wa mwisho, awe Idriss Mbombo au Prince Dube. Safu ya Kiungo cha ushambuliaji huwa inakamilishwa na Abdul Sopu, Kipre Junior, Djibril Sylla, Alassane Diao, Iddy Nado na Ayoub Lyanga. Wana utajiri sana eneo hili ndio maana kazi kubwa itakuwepo kwenye kiungo. Sospeter Bajana na Akaminko wanatarajiwa kuwepo kuwapa ulinzi safu yao ya Ulinzi, ikiwa na Lusajo Mwaikenda, Cheikh Sidibe, Malickou Ndoye na Nahodha Daniel Amoah kumlinda Idrissu kwenye mechi 2 mfululizo.

Yanga wanafahamu umuhimu wa kushinda mchezo wa leo na licha ya Mwalimu Gamondi kusema kuwa haangalii matokeo ya wengine kuwa nani kafanya nini, lakini ni dhahiri anafahamu kutopata ushindi kwenye mchezo wa leo, kutamuweka kwenye wakati mgumu hata kama ni mwanzo wa msimu.

Dabo anatarajiwa pia kuutumia mchezo wa leo kurudi kileleni mwa Msimamo na atatumia kila silaha aliyokuwa nayo kukamilisha azma yake ya ushindi. Tayari kaonja joto ya jiwe ya Yanga msimu huu baada ya kufungwa 2-0 kwenye mechi ya Ngao ya jamii, na bila shaka atataka kujiuliza.

Bonge la mechi kwa Mkapa, rekodi za Yanga dhidi ya Azam zinaibeba sana Yanga kupata ushindi leo lakini pia ushindi wa 3-0 dhidi ya Geita baada ya kupoteza 2-1 kwa Ihefu imeirudisha timu kwenye morali yake. Azama wakishindi mechi mbili ngumu mfululizo. Utamu wa mechi utakuwa kwenye eneo la Kiungo. Tunatarajia kuona viungo wengi sana wakitifuana eneo hili, ila kwa namba za kitakwimu za viungo wa Yanga, Azam kashikwa pabaya.

Makala Nyingine

More in Azam FC