Beki wa zamani wa Liverpool Mamadou Sakho inasemekana alimshambulia meneja wa Montpellier Michel Der Zakarian baada ya mazoezi Jumanne jioni, na sasa yuko katika hatari ya kutimuliwa na klabu hiyo ya Ufaransa. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 alikaa kwa miaka minane katika ligi kuu ya nchini Uingereza, huku minne kati ya hiyo akiitumukia Liverpool na baadae aliondoka na kujiunga na Crystal Palace 2017. Alirudi Ufaransa kusaini Montpellier mnamo 2021, lakini siku zake za kucheza Ligue 1 zinaweza kuhesabiwa baada ya mabishano makali na meneja wa timu hiyo.
Kulingana na ripoti, Sakho alimshika Der Zakarian kwenye kola na kumwangusha chini mbele ya wachezaji waliokuwepo katika uwanja huo wa mazoezi, ripoti hiyo imeeleza kuwa katika mazoezi ya jana (Jumanne) jioni Sakho alitoka nje ya uwanja wa mazoezi (alisusa) baada ya kutopewa faulo, kisha kocha huyo akamzomea na kumuita “Cry-Baby” ndipo Sakho alipojibu kwa kumshika shati na kumsukuma hadi chini. Ugomvi uliendelea hadi wachezaji wengine walipoingilia kati.
Si Sakho wala Der Zakarian waliokuwa tayari kuzungumza zaidi kuhusu suala hilo, Sakho anaweza kufutwa kazi kwa utovu wa nidhamu ikiwa klabu itagundua kuwa kulikuwa na viashiria vya utovu wa nidhamu. Aliambiwa hakuwa tena sehemu ya mipango ya Der Zakarian katika majira ya joto, lakini hakuweza kupata uhamisho mahali pengine. Mfaransa huyo amecheza kwa muda mfupi tu kama mchezaji wa akiba kwenye ligi msimu huu na hiyo inaweza kuwa mechi yake ya mwisho kuitumikia klabu hiyo.
Montpellier wamekuwa na mwanzo mgumu msimu huu baada ya kuambulia pointi tisa pekee kutoka kwa mechi nane za mwanzo huku wakiwa wanashika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi kuu nchini Ufaransa (ligue 1). Pia walikuwa na mechi dhidi ya Clermont Foot ilioahirishwa mapema mwezi huu baada ya kipa wa timu pinzani kulengwa na fataki iliyorushwa na mashabiki. Kipa wa Clermont Foot, Mory Diaw alitolewa nje, huku mwenzake Neto Borges akionyeshwa kadi nyekundu kwa kutoa ishara ya kidole cha kati kwa mashabiki wa Montpellier. Mchezo huo ulisitishwa kwa muda ulioongezwa, na Montpellier wamejipanga kukabiliana na tabia ya mashabiki wao hivi karibuni.