Connect with us

NBC Premier League

MUDATHIR YAHAYA KUIKOSA KARIAKOO DERBY?

Wachezaji wawili wa Yanga na Azam FC watarajie rungu la Tsh.500,000 (laki tano) na kufungiwa mechi tatu kutoka bodi ya ligi kutokana na kitendo walichokifanya kwenye mchezo wa juzi, Jumatatu huku presha kubwa ikiwa kwa Yanga ambao wanaweza kumkosa kiungo wao Mudathir Yahaya Abas kwenye mechi yao ya ligi ya NBC dhidi ya watani zao Simba itakayochezwa Jumapili ya Novemba 5 mwaka huu katika uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kwa mujibu wa kanuni ya 41:5 (5.4), kufanya kitendo chochote cha aibu, kama vile kukojoa uwanjani, kukataa kupeana mkono na mgeni rasmi, waamuzi na wachezaji wa timu pinzani, kutoa au kuonyesha ishara inayoashiria matusi ni kosa.

Feisal Salum wa (Azam FC) na Mudathir Yahya wa (Yanga) wamezua taharuki kwa kutegeana kuingia eneo la kuchezea la Uwanja wa Benjamin Mkapa. Tukio hilo lilitokea wakati vikosi vya timu hizo vikiingia uwanjani hapo tayari kuanza dakika 45 za kipindi cha kwanza na wachezaji hao walisimama kwenye mstari wa kuingia eneo la kuchezea.

Feisal Salum (Fei Toto) alikuwa anafanya mazoezi ya viungo kwa kunyoosha miguu huku Mudathir akikung’uta viatu vyake ili kuvuta muda wa nani awahi kuingia uwanjani kitendo ambacho bodi ya ligi inatafsiri kama imani za kishirikiana na kutoza faini.

Mastaa hao walikuwa nje kwa muda wakati wachezaji wenzao wakijipanga na kusalimiana, Feisal na Mudathir waliendelea kutegeana hadi zoezi hilo lilipokamilika huku kila kikosi kikienda upande wake. Wakati taharuki kwa mashabiki ikiwa kubwa baada ya kushtukia kitendo hicho, ndipo Mudathir alipoamua kuwa wa kwanza kwenda kuungana na wenzake huku Feisal naye akifuata na kupiga picha za vikosi.

Kumbukumbu za mashindano ya ligi kuu ya NBC msimu uliopita wachezaji wa Simba na Yanga Aziz KI na Clatous Chama, walilipishwa faini ya Tsh.500,000 (laki tano) na kufungiwa kutokucheza mechi tatu za Ligi Kuu zilizokuwa zinafuata kwa kosa kama hilo.

Makala Nyingine

More in NBC Premier League