Connect with us

Top Story

TWIGA STARS KUSHUKA DIMBANI LEO.

Timu ya Taifa ya Tanzania Twiga Stars kushuka dimbani hii leo saa 12:00 Jioni kuikabili Botswana katika mchezo wa marejeano, mchezo wa kwanza Tanzania ilishinda 2-0 nyumbani

Timu ya Taifa ya Tanzania Twiga Stars inashuka Dimbani hii leo dhidi ya timu ya Taifa ya Botswana katika Jiji la Gaborone nchini Botswana majira ya saa 12:00 Jioni katika mchezo wa marejeano wa kuwania nafasi ya kufuzu Olympic 2024 nchini Ufaransa.

Kuelekea mchezo huo kocha mkuu wa kikosi hicho Bakari Shime amelalamikia hali ya uwanja ambao watautumia hii leo kuwa haufai kwaajili ya mchezo licha ya kwamba amewaandaa vijana wake kupambana kwenye hali zote.

Aina ya mechi ambayo tunacheza na ubora wa kiwanja ni vitu viwili tofauti, kwa aina ya uwanja ulivyo kama itanyesha mvua maana yake kutakuwa na hali mbaya sana kwenye huu uwanja, lakini yote kwa yote inawezekana ni mipango ya timu mwenyeji kutuleta hapa kucheza katika uwanja huu, tutajipanga vizuri tucheze kulingana na mazingira ya kiwanja lakini mwisho wa siku tuweze kulinda matokeo yetu tupate matokeo zaidi na kusonga mbele.

Bakari Shime Kocha mkuu wa kikosi cha Twiga Stars.

Nahodha wa kikosi cha Twiga Stars Julieth Singano amesema kwa upande wa wachezaji wamejipanga vizuri kuhakikisha wanapata matokeo katika mchezo huu wa leo

Natumaini tutafanya vizuri kwa kuwa wachezaji tupo na morali na hali ya juu katika mchezo huu, tunaomba sapoti yenu Watanzania kwa dua zenu ili tufanye vizuri kulinda ushindi wetu.

Julieth Singano, Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania Twiga Stars.

Kama Tanzania itafanikiwa kufuzu katika hatua hii huenda ikakutana na timu ya Taifa ya Nigeria kwenye hatua inayofuata.

Makala Nyingine

More in Top Story