Michuano ya African Football League imefikia hatua ya fainali baada ya jana kushuhudia michezo miwili ya nusu fainali ikichezwa katika viwanja viwili tofauti Barani Afrika.
Mchezo wa mapema ulikuwa ukiikutanisha Esperance de Tunis ikiwa nyumbani dhidi ya Wydad Casablanca, mchezo ambao uliamuliwa kwa changamoto ya mikwaju ya penalty baada ya dakika 90 kutamatika Esperance wakiwa mbele kwa 1-0 goli lililofungwa na Rodrigues Silva na matokeo ya jumla kuwa 1-1, na katika mikwaju ya penalty Wydad ikashinda 4-5 na kusonga mbele.
Mchezo wa nusu fainali ya pili uliihusisha Al Ahly dhidi ya Mamelodi Sundowns, mchezo wa awali ulitamatika kwa Mamelodi kuibuka na ushindi wa goli 1-0 wakiwa nyumbani, hii ilikuwa ni moja ya mechi bora zaidi kupigwa Barani Afrika, kabla ya mchezo huu wa marejeano Al Ahly waliandika barua kuelekea shirikisho la soka Afrika kuhusu maamuzi ya waamuzi kuwa na upendeleo.
Al Ahly waliingia wakihitaji kupata goli la mapema zaidi, walilishambulia kwa kasi sana lango la Mamelodi Sundowns hadi wakapata Penalty iliyopigwa na Ali Maaloul na kuokolewa na golikipa Ronwen Williams. Mamelodi Sundowns walicheza kwa utulivu sana katika dakika zote licha ya kushambuliwa sana na kosa kosa nyingi langoni kwao.
Zikiwa zimesalia dakika sita (6) kabla ya dakika 90 Mandieta Junior nyota wa Mamelodi Sundows aliyeingia akitokea benchi alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu mbaya nyota wa Al Ahly Tawfik, hii pia haikuwatoa mchezoni Mamelodi hadi dakika zote 90 zinamalizika matokeo ilikuwa 0-0, matokeo ya jumla kuwa 0-1 ambayo yaliifanya Mamelodi Sundowns ifuzu hatua ya fainali ya AFL.
Fainali ya African Football League itaikutanisha Wydad AC dhidi ya Mamelodi Sundowns.