Uchaguzi wa UFA uliofanyika leo na kummpa kura zote za Ndio ndugu Mohamed Sozigwa kuwa Mwenyekiti wa UFA na Ndugu Bakari Kisu kuwa Makamu Mwenyekiti wa UFA, kati ya kura 46, zilizopigwa na Wajumbe 46 wanachama wa UFA, umepingwa vikali na baadhi ya wajumbe wa chama hicho wakidai kuwa ni batili na umefanyika Kihuni.
Wakiongea baada ya uchaguzi huo baadhi ya wajumbe hao walikuwa na haya ya kusema.
Hatuutambui uchaguzi huu na tunasikitishwa na kilichofanyika. Wajumbe waliopiga kura tunawafahamu sio wanachama wa UFA ni vikundi tu wawa watu waliojikusanya kuja kufanya mambo kwa ajili ya maslahi yao. Mimi ndio Katibu wa vilabu vyote wilaya ya Ubungo, vilabu vipo 22 na ninachofahamu hakuna kiongozi hata mmoja wa hivyo vilabu aliyekuwepo.
Alisema Edgar Katembo, Katibu wa Mabibo Boys
Tunachofahamu sisi, uchaguzi ulisimamishwa na tukapewa maelekezo kuwa tukae kamati tendaji kujadili namna bora ya kuliendea hili na mkutano ulishapangwa ufanyike tarehe 7, Landmark Hotel lakini tumeshangazwa kuona wameokotana leo na kufanya uchaguzi. Sisi hatuutambui uchaguzi huu. Kwanza nafasi zinazogombewa sio mbili tu, zipo nyingine na hazijatangazwa. Watu wenye nia ovu na soka letu wamelazimisha uchaguzi kufanyika leo.
Aliongeza Katembo.
Mjumbe mwingine, Nassoro Maligwa, Katibu wa Mugabe FC ya Sinza, naye alieleza masikitiko yake na kusema kuwa hii ni hatari kwa afya ya soka letu.
Kilichofanyika leo ni uhuni tu. Katibu wa Wilaya wa chama alishatupa barua za kuusogeza mbele uchaguzi. Waliokuja kupiga kura leo wengi tunawafahamu sio wa huku ni wa wilaya zingine lakini wamekuja kupiga kura kwetu. Sasa hii ni hatari sana kwenye maisha ya mpira.
Alipotafutwa mwenyekiti wa kamati ya Uchaguzi kutoka DRFA, ndugu Yusuf Ayubu alikuwa na haya ya kusema
Uchaguzi ulikuwa wa huru na haki na wala hapakuwa na changamoto yoyote. Kura zote 46 zilipigwa kwa Mwenyekiti -46 na hakuna iliyoharibika na hata kwa Makamu Mwenyekiti pia. Wanaosema uchaguzi huu ni batili walitakiwa waje waangalie mchakato ndipo walalamike. Mimi nilienda kwa ajili ya kusimamia akidi tu, nimeangalia ledger yao nikaithibitisha na uchaguzi ukafanyika, sasa hayo mengine ni taarifa tu kama taarifa zingine.
Taarifa zinasema kuwa Mkuu wa wilaya ya Ubungo alishatoa muongozo kuwa uchaguzi huu usogezwe mbele mpaka Novemba 7 ili kwanza kuweka maandalizi na mambo mengine sawa kabla ya kuendelea na mchakato kwenye kikao walichokaa jana ofisini kwake.
Kufanyika uchaguzi leo ni kile kinachodaiwa kama ukiukwaji wa maagizo.
Endelea kukaa nasi kwa taarifa zaidi juu ya sakata hili