Connect with us

NBC Premier League

CHAMA: TUSILAUMIANE, TUUNGANE PAMOJA.

Klabu ya Simba imekuwa kwenye mzozo na mgogoro mkubwa baada ya kupokea kichapo cha magoli 5-1 kutoka kwa mtani wake wa karibu klabu ya Yanga katika mchezo wa Ligi kuu kandanda Tanzania Bara, wanachama wa klabu hiyo kupitia vyombo mbalimbali vya habari wameonekana wakitoa mashinikizo ya kujihudhuru kwa mwenyekiti wao Murtaza Mangungu na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi Salim Abdallah “Try Again”.

Hadi hivi sasa klabu hiyo imefikia makubaliano ya kuachana na aliyekuwa kocha wa kikosi hicho Roberto Oliviera pamoja na aliyekuwa kocha wa viungo wa klabu hiyo. kwasasa klabu hiyo inaongozwa na kocha wa mpito Daniel Cadena akishirikiana na Suleiman Matola.

Lakini pia baada ya kupata matokeo hayo mabaya zaidi kwa upande wa klabu ya Simba shutuma zikatolewa zikidai kuwa baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo waliuza mchezo huo kwa maana ya kupokea rushwa kutoka upande wa klabu ya Yanga jambo ambalo lilifika hadi Bungeni jana na kutolewa ushauri na wabunge kuwa klabu hiyo kufika ofisi za TAKUKURU Manispaa ya Temeke kushitaki jambo hilo.

Kiungo mshambuliaji wa klabu ya Simba raia wa Zambia Clatous Chota Chama kupitia ukurasa wake wa Instagram amewataka mashabiki na wanachama wa klabu ya Simba kutokunyosheana vidole na badala yake watulie na wawe kitu kimoja kuelekea katika michezo inayofuata.

Kwenye kipindi hiki hakuna haja ya kunyosheana vidole na kuhamisha majukumu, haitatusaidia kwa namna yoyote ile.

Huu ndio wakati sahihi wa kushikamana, kuiweka mioyo na vichwa vyetu pamoja kusonga mbele pamoja.

Twendeni tena leo tukiwa na ari tukafanye kazi kwaajili ya kujikomboa sisi wenyewe

Clatous Chota Chama, Mchezaji wa klabu ya Simba.

Nahodha wa kikosi cha Simba Mohamed Hussein kupitia ukurasa wake wa Instagram pia amesema yaliyotokea yamewafanya wajifunze na wamechukua hatua kwenda mbele na amewaomba wapenzi na mashabiki wa Simba kufika kuwashangilia mara zote wawapo uwanjani katika michezo ijayo.

Hatujawa na wakati mzuri kwa siku za karibuni lakini lazima tukubali kwamba yameshatokea, tumejifunza na kuchukua hatua kwenda mbele ambako safari bado ni ndefu. Umoja wetu kama ilivyo #NguvuMoja ni muhimu kwetu wote tukianza na leo kwa kuja uwanjani kutushangilia.

Mohamed Hussein, Nahodha na mlinzi wa klabu ya Simba ameandika kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Simba inashuka dimbani tena leo saa 10:00 Jioni kuikabili Namungo katika mwendelezo wa michezo ya Ligi kuu Tanzania Bara.

Daniel Cardena Kocha wa mpito wa klabu ya Simba.
Suleiman Matola kocha wa mpito wa klabu ya Simba.

Makala Nyingine

More in NBC Premier League