Connect with us

NBC Premier League

SIMBA YABANWA MBAVU NA NAMUNGO.

Simba wanalazimishwa sare ya 1-1 na Namungo kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Uhuru na kufikisha alama 19 baada ya michezo 8 kabla ya kuelekea kwenye dirisha la kalenda ya kimataifa.

Namungo walitangulia kupata goli kupitia kwa Reliants Lusajo dakika ya 32 akitumia uzembe wa mabeki wa Simba kuondosha mpira uliokuwa ukizengea kwenye eneo lao.

Simba walipata goli la kusawazisha dakika ya 75 kupitia kwa Jean Othos Baleke akimalizia kazi nzuri iliyoanzishwa na Luis Miquissone kabla ya pasi ya usaidizi kutoka kwa Mzambia Moses Phiri.

Wakitoka kwenye kupoteza dhidi ya watani wao Yanga, Simba ilionekana kuumiliki mchezo muda mwingi kuanzia dakika ya 1 ya mchezo lakini ilikosekana kasi ya kushambulia na kutengeneza nafasi za magoli hali iliyowafanya Namungo kuanza kujiamini na kufika langoni kwa Simba hadi walipotengeneza nafasi ya bao.

Ilimmlazimu mwalimu wa Simba, Cadena kufanya mabadiliko mengi ya kiushambuliaji kipindi cha pili ili aweze kukomboa bao hilo, akiwaingiza Moses Phiri, John Bocco, Luis Miquissone, Shabani Chilunda.

Namungo walipambana sana kulilinda lango lao, Derrick Mukombozi na Erasto Nyoni hasa wakifanya kazi kubwa kummlinda Jonathan Nahimana.

Simba walijaribu kufanya kila jitihada kupata matokeo lakini bado hayakuwa upande wao. Pengine hata Namungo wangekuwa watulivu wangeweza kuondoka na matokeo leo. Simba bado hawakuwa kwenye ubora wao.

Baada ya Mchezo walimu wote wawili waliongea

” Ukiniuliza siku 2 zilizopita kama hii sare nitaifurahia ningesema ndio lakini kwa namna tulivyocheza na kutengeneza nafasi kadhaa za kumaliza mechi, naweza sema nimesikitishwa na sare hii, tulistahili kushinda hii mechi. Lakini nawasifu vijana wangu wamecheza ndani ya mpango wetu vizuri.” Denis Kitambi, Kocha Namungo.

Naye Dani Cadena alikuwa na haya ya kusema

“Tulitamani kushinda mchezo huu na nakiri tulikuwa chini sana lakino bado wachezaji walipambana kupata hii alama 1. Ilinilazimu kuingiza washambuliaji wengi kwakuwa tulikuwa nyuma kwa goli 1. Nadhani wachezaji wataenda kupumzika kwa siku kadhaa wasahau kidogo kuhusu mpira ili warudi wakiwa timamu na kuendelea na michezo ijayo.”

Simba wanapata sare yao ya kwanza msimu huu baada ya kushinda michezo 6 na kufungwa 1 Kwenye michezo yao 8 ya msimu huu hadi sasa.

Makala Nyingine

More in NBC Premier League