Connect with us

CAF Women Champions League

JKT QUEENS YAONDOSHWA CAFWCL.

Klabu ya JKT Queens kutoka Tanzania usiku wa kuamkia leo imeondoshwa rasmi katika michuano ya Ligi ya mabingwa Barani Afrika kwa upande wa wanawake inayoendelea nchini Ivory Coast baada ya kukubali kichapo cha goli 4-1 kutoka kwa Sporting Club Casablanca ya Morocco.

JKT Queens waliingia katika mchezo huo wakiwa wanajiamini baada ya kupata ushindi na kuvuna alama tatu (3) katika mchezo uliopita wa 2-1 dhidi ya Athletico d’Abidjan ya Ivory Cost, hivyo waliingia wakiwa katika nafasi ya pili ya msimamo nyuma ya Mamelodi Sundowns Ladies waliokuwa na alama 6 kabla hawajapata ushindi jana.

CS Casablanca waliingia katika mchezo huu wakiwa wametoka kupoteza katika mchezo wao dhidi ya Mamelodi Sundowns kwa goli 1-0 na hivyo kuwa nafasi ya tatu (3) na alama moja (1) waliyoipata baada ya kutoka sare na Athletico Abidjan katika mchezo wa kwanza.

Mchezo ulikuwa umejaa hisia nyingi, ulikuwa ni kama mchezo wa fainali kwani kila timu ilikuwa inahitaji ushindi, Dakika ya 29 ya mchezo mlinzi kitasa wa JKT Queens Happiness Hezron Mwaipaja alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kufanya madhambi ndani ya eneo la 18 na timu yake kuadhibiwa kwa mkwaju wa penalty.

Baada ya kadi hiyo nyekundu mafuriko ya magoli yalianza kuiandama JKT Queens huku ikimuacha Kocha wa kikosi hicho Esther Chaburuma asijue nini afanye, dakika ya 30 Meryem Hajri akaiandikia goli la kwanza timu ya CS Casablanca kwa mkwaju wa penalty.

Dakika ya 39 CS Casablanca wakaandika tena goli la pili kupitia kwa Chaymaa Mourtaji baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Nadege Koffi, na dakika ya 45 vijana wa CS Casablanca wakaandika goli la tatu kupitia kwa Nadege Koffi aliyepokea pasi mujarabu kutoka kwa Salma Tammar. Hadi mapumziko CS Casablanca 3-0 JKT Queens.

Kipindi cha pili vijana wa JKT Queens walianza kwa kasi kulishambulia lango la CS Casablanca licha ya kuwa pungufu uwanjani na dakika ya 56 wakaandika goli la kufutia machozi kupitia kwa Stumai Abdullah aliyepokea pasi mujarabu kutoka kwa Eto Mlenzi.

Jahazi la vijana wa JKT Queens lilizidi kuzama zaidi baada ya CS Casablanca kujipatia goli la nne (4) dakika ya 58 kupitia kwa Syliviane Kokora akipokea pasi nzuri kutoka kwa Aicha Samake ambaye alihitimisha karamu ya magoli kwa upande wa CS Casablanca usiku wa jana. Dakika ya 74 JKT Queens walifanya mabadiliko kwa kumtoa Fatma Makusanya na kumuingiza Kadosho Shekigenda.

Dakik ya 85 ya mchezo mchezaji wa JKT Queens, Anastazia Nyandago Simba akaonyeshwa kadi nyekundu, na hii ikawa kadi ya pili nyekundu kwa JKT Queens katika mchezo wa jana na hivyo kulazimika JKT Queens kumaliza mchezo huo wakiwa 9 uwanjani.

Vijana walipambana kwa kadri ya uwezo wao na wameipeperusha vyema bendera ya Tanzania na Afrika mashariki, lakini jana waliikosa huduma ya mshambuliaji wake nyota Winfrida Gerald na nyota wengine waliopo katika kikosi cha timu ya Taifa ya wanawake chini ya miaka 20,

KIKOSI KILICHOANZA JANA KWA UPANDE WA JKT QUEENS.

  • Najiat Idrisa Abass Jezi no; 18
  • Anastazia Nyandago Simba Jezi no; 5
  • Esther Mabanza Gindulya Jezi no; 3
  • Voleth N. Mwamakamba Jezi no; 11
  • Happiness H. Mwaipaja Jezi no; 19
  • Alia Fikiri Salum Jezi no; 14
  • Stumai Abdallah Athumani Jezi no; 8
  • Janeth c. Pangamwene Jezi no; 10
  • Eto Hamisi Mlenzi Jezo no; 16
  • Donisia Daniel Minja Jezi no; 6
  • Fatma Bashiru Makusanya Jezi no; 17.

Jana JKT Queens ilikuwa na benchi finyu sana la ufundi likiwa na wachezaji wanne pekee kwenye benchi na katika mchezo mzima wamefanya mabadiliko mara moja pekee, hii pengine imepelekewa na nyota wake sita (6) kuondoka kambini kwaajili ya majukumu ya timu ya Taifa na wengine kuwa wagonjwa. Wachezaji waliokuwa wamesalia kwenye benchi ni;

  • Kadosho Shabani Shekigenda Jezi no; 13
  • Asha Ismail Mrisho Jezi no; 20
  • Anastazia Antony Katunzi Jezi no; 2
  • Amina Ally Bilali Jezi no; 4

Makala Nyingine

More in CAF Women Champions League