Denver Nuggets Jana waliinyuka Los angeles Clippers vikapu 111-108 kwenye mchezo wa makundi ya NBA Play In-Season Tournament na kupata ushindi wao wa 9 msimu huu.
Licha ya kuwa na majina makubwa kama, Paul George, Kahwi Leonard, James Harden na Russel Westbrook, LA Clippers bado waliangukia pua mbele ya Mwamba Nikola Jokic aliyefunga vikapu 32, akirejesha mipira mara 16 na kutoa pasi za usaidizi 9 huku akifuatiwa kwa karibu na Kentavious Caldwel-Pope.
Denver Nuggets wanaonekana kuwa na jambo lao msimu huu kwani wamepoteza michezo 2 tu msimu huu hadi sasa, licha ya kuwa bado mapema.
Matokeo mengine ya jana ni kama ifuatavyo:-
Golden State Warriors wakimmkosa Steph Curry walifungwa jana vikapu 104 -101 na Minnesota Timberwolves. Draymond Green na Klay Thomson wakishindwa kuokoa jahazi. Uttah Jazz walipata ushindi wao wa 4 msimu huu wakifunga Portland Trail Blazers kwa vikapu 115-99. Brooklyn Nets wakiwa nyumbani waliadhibu Orlando Magic 124-104.
Washindi wakubwa wa jana ni pamoja na New Orleans Pelicans wakiwchapa 131-110 Dallas Mavericks. Brandon Ingram akifunga vikapu 25 na Zion Williamson akifunga vikapu 19 vilisaidia kuwazima Kyrie Irving(17), Luka Doncic(16) na wenzao.
LeBron James alirejea kikosini jana na kuiongoza Lakers kupata ushindi wake wa 6 msimu huu wakiwafunga Memphis Grizzlies vikapu 134-107. Shoo ilisimamiwa vema na vijana D’angelo Russel aliyefunga vikapu 24, kurejesha mipira 3 na pasi za usaidizi 5. Rui Hachimura akifunga vikapu 23 na Antony Davis akifunga vikapu 19 kupeleka msiba huo kwa Grizzlies.