Wakiendelea kummkosa mfungaji wao tegemeo Steph Curry kutokana na majeraha ya goti aliyoyapata kwenye mchezo waliofungwa 116-110 na Timberwolves Jumapili, na mchezaji wao mwingine mahiri Draymond Green anayetumikia adhabu ya kifungo cha mechi 5 na huku Klay Thomson akicheza chini ya kiwango akifunga vikapu 5 tu kwenye dakika 27 alizocheza, Warriors walionekana kama kuku aliyekatwa kichwa mbele ya Oklahoma City Thunder.
Thunder, walirekodi ushindi wao wa 8 wa msimu huu baada ya kuwanyuka wapinzani wao Warriors kwa vikapu 128-109. Alikuwa ni Shai-Gilgeous Alexander akiendelea kuwa na msimu bora kabisa akifunga vikapu 24, akirejesha mipira 2 na kutoa pasi za usaidizi 7 pamoja nae Isaiah Joe aliyefunga vikapu 23 ndio walikuwa vinara wa kupeleka taabu kwenye taabu za Warriors
Jonathan Kuminga(21), Andrew Wiggins(12), Chris Paul(15), Kevon Looney(13) walifungia vikapu Warriors lakini havikuweza kusaidia kuiokoa timu kutoka kwenye kichapo. GSW wanapoteza mchezo wao wa 7 msimu huu na kushinda michezo 6. Pengine miongoni mwa misimu iliyoanza vibaya kwa wamba hawa wa San Fransisco.
Kwingineko, Jijini Miami, Muunganiko wa Jimmy Butler, Bam Adebayo na Duncan Robinson umeendelea kuwa tishio ukiwapelekea Brooklyn Nets “Heat” ya kutosha kwa kuwachabanga vikapu 122-115. Butler alifunga vikapu 36, Robinson vikapu 26 na Adebayo vikapu 20 kuhakikishia Miami Heat wanaibuka na ushindi huo wa 8 msimu huu.