Connect with us

Taifa Stars

STARS KUSHUKA DIMBANI LEO DHIDI YA NIGER.

Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ itashuka dimbani hii leo majira ya saa moja jioni [19:00] kukipiga dhidi ya timu ya Taifa ya Niger katika uwanja wa Grande Marrakech Annex nchini Morocco kwenye mchezo wa kwanza wa kundi E wa kusaka tiketi ya kufuzu fainali za kombe la Dunia.

Taifa Stars inaundwa na nyota wengi wanaocheza soka la kulipwa nje ya mipaka ya Tanzania wakiongozwa na nahodha wa kikosi hicho Mbwana Ally Samatta anayekipiga PAOK, Simon Msuva na nyota wengine kibao.

Mkuu wa msafara wa kikosi hicho ambaye pia ni Rais wa shirikisho la soka visiwani Zanzibar, Dkt Suleiman Jabir amesema kikosi kinaendelea vizuri na mazingira ya mchezo yapo vizuri na ari ya wachezaji ipo juu kuelekea mchezo huu.

Vijana wanaonekana wanaitaka mechi na kwa umuhimu wake ni kufuzu kucheza kombe la Dunia la 2026, Tunafahamu tuko kwenye group ambalo lina timu nzuri, Niger, Morocco, Zambia na Congo.

Tupo kwenye kundi ambalo kama tutajipanga vizuri na vijana kufata maelekezo ya mwalimu vizuri pamoja na kuongeza juhudi na maarifa na ari ya kweli, tunaimani kuwa tunaweza kuandika historia ya kucheza fainali za kombe la Dunia 2026.

Ombi langu kwa Watanzania waiombee timu yetu na kuombea ushindi ili tuweze kushinda mchezo huu kwasababu kushinda mchezo huu wa kwanza itatupa dira nzuri.

Dkt. Suleiman Jabir, Rais wa ZFF na mkuu wa msafara wa Taifa Stars.

Kocha mkuu wa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania Adel Amrouche amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ndege ambayo wamesafiria kuelekea nchini Morocco.

Namshukuru Rais Samia kwa kutupatia usafiri, kama tusingekuwa na hiyo ndege naamini tungeteseka sana, Afrika kusafiri kutoka Mashariki kwenda Magharibi ni ngumu sana.

Tunaenda kufanya kila kitu ili kuwafanya watu wafurahi, kwangu mimi mpira ni mpira lakini kuwafanya watu wafurahi ndio kipaombele changu.

Adel Amrouche, kocha mkuu wa kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania.

Baada ya mchezo wa leo Jumamosi kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania kitaanza safari ya kurejea nchini kwaajili ya mchezo dhidi ya Morocco ambao utapigwa Jumanne ya wiki ijayo November 25.

Kila lakheri Taifa Stars.

Makala Nyingine

More in Taifa Stars