Connect with us

CAF Women Champions League

MAMELODI MABINGWA LIGI YA MABINGWA AFRIKA.

Ligi ya mabingwa Barani Afrika kwa upande wa wanawake iliyokuwa inafanyika nchini Ivory Coast imetamatika jana kwa klabu ya Mamelodi Sundowns kutangazwa kuwa mabingwa kwa mara ya pili tangu michuano hii ianzishwe.

Mamelodi Sundowns Ladies wamekuwa mabingwa jana baada ya kuibuka na ushindi wa goli 3-0 dhidi ya Club Sporting Casablanca ya Morocco. Hii ni mara ya pili kwa timu hizi kukutana katika michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika msimu huu baada ya kukutana tena katika hatua ya makundi ambapo Mamelodi Ladies waliibuka na ushindi wa goli 1-0.

CS Casablanca ilikuwa ni mara yake wa kwanza kushiriki kwenye michuano hii na ilipangwa Kundi A sambamba na klabu mwenyeji Athletico d’Abidjan, klabu kutoka Tanzania JKT Queens ambayo iliondoshwa hatua ya makundi pamoja na Mamelodi Sundowns.

CS Casablanca ilifika fainali baada ya kuiondosha klabu ya Ampem Darkoa ya Ghana katika hatua ya nusu fainali na Mamelodi Sundowns walifika hatua ya fainali baada ya kuichapa FAR Rabat ya Morocco katika hatua ya nusu fainali.

Magoli mawili ya mfungaji bora wa michuano hii Tholakele Refilwe na goli la Boitumelo Rabales yalitosha kuwahakikishia vijana wa Mamelodi Sundowns Ladies ubingwa nchini Ivory Coast mbele ya CS Casablanca ya Morocco wakilibeba taji ambalo walishindwa kulitetea msimu uliopita mbele ya FAR Rabat.

Mamelodi Sundowns Ladies imebeba ubingwa huu bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa katika michezo yote mitano (5) ambayo timu hii imecheza. Mchezo wa fainali ulipigwa katika dimba la Gon Colulibaly uliopo Korhogo Jumapili jioni.

Mamelodi Sundowns Ladies bila kupoteza muda katika mchezo wa fainali walipata goli dakika ya 21 kwa mkwaju wa Penati uliowekwa kimiani na Tholakele Refilwe.

Dakika chache baadae kabla ya mapumziko, Boitumelo Rabales aliiandikia goli la pili Mamelodi Sundowns baada ya kumalizia vyema mpira akiwa ndani ya eneo la kisanduku, goli ambalo liliipeleka Mamelodi Sundowns mapumziko ikiwa inaongoza goli 2-0.

Kipindi cha pili kiliporejea mashambulizi ya hatari yaliendelea kufanywa na timu zote mbili lakini CS Casablanca mara nyingi walikutana na ukuta mgumu wa Mamelodi Sundowns na dakika ya 78 ya mchezo Mamelodi Sundowns wakaandika goli la tatu na la ushindi kupitia kwa nyota wake Tholakele Refilwe.

Hadi mchezo unamalizika Mamelodi Sundowns Ladies 3-0 CS Casablanca na Mamelodi wakatangazwa kuwa mabingwa kwa mara nyingine tena wa Ligi ya mabingwa Barani Afrika na kukabidhiwa kitita cha $ 400,000.

Baada ya mchezo huo kumalizika kocha mkuu wa kikosi cha Club Sporting Casablanca aliwapongeza Mamelodi Sundowns Ladies kwa kutwaa ubingwa huu.

Ulikuwa uzoefu mzuri kwenye timu hii leo, ningependa kuwapongeza Mamelodi Sundowns kwa ushindi. Wamecheza vizuri sana na walikuwa bora sana.

Haya yalikuwa mashindano makubwa kitu ambacho ni kizuri kwa soka la wanawake Afrika.

Mehdi El Qaichori, kocha mkuu wa Club Sporting Casablanca.

Jerry Tshabalala kocha mkuu wa kikosi cha Mamelodi Sundowns Ladies nae ameeleza furaha yake baada ya kuibuka na ushindi ulioambatana na ubingwa mbele ya CS Casablanca.

Ukiniona ninafuraha, ujue naitoa kwa wachezaji wangu. Wachezaji wenye furaha siku zote wataleta matokeo mazuri kwenye timu. Tunataka kuendelea kufanya vizuri.

Sasa malengo yetu tunaamini siku moja tutakuwa na kombe la klabu la Dunia la wanawake na tutaenda kuiwakilisha Afrika kama mabingwa wa Afrika.

Jerry Tshabalala, kocha wa Mamelodi akiamini siku moja kutafanyika mashindano ya Dunia na watawakilisha kama mabingwa.

Golikipa Bora wa mashindano hayo Andile Dlamini baada ya kuchukua ubingwa wa Ligi ya mabingwa Afrika alisema tuzo hiyo inaenda kwa wasichana wadogo ambao waliwaamini wao.

Tumefanya kwaajili yenu, tumefanikiwa kwaajili ya vijana wadogo wa kike waliotuamini, hatuzungumzi sana lakini tunafanya kazi uwanjani, hivyo ndivyo tulivyo, sisi ni Mamelodi Sundowns, sisi ni waafrika Kusini, na tunajivunia, ahsanteni sana Ivory Coast na watu wenu mko vizuri.

Andile Dlamini.

Tuzo mbalimbali zilitolewa kwa timu zilizofanya vizuri kwenye mashindano hayo.

  • Mamelodi Sundowns – Mabingwa
  • CS Casablanca – Mshindi wa pili
  • FAR Rabat – Mshindi wa Tatu
  • Tholakele Refilwe – Mfungaji Bora [Mamelodi Sundowns]
  • Boitumelo Rabale – Mchezaji Bora [Mamelodi Sundowns]
  • Andile Dlamini – Golikipa Bora [Mamelodi Sundowns]
  • Mamelodi Sundowns – timu yenye mchezo wa kiungwana [Fair Play Team].

Makala Nyingine

More in CAF Women Champions League