Kiungo wa timu ya Taifa ya Tanzania [Taifa Stars] na klabu ya Azam FC, Sospeter Bajana amesema kitendo cha kufuatwa na kuombwa jezi na nyota wa timu ya Taifa ya Morocco na klabu ya Manchester United Sofyan Amrabat hakukitarajia kabisa.
Sikutarajia kama Amrabat angeniomba jezi, lakini alinifuata mwenyewe na kupiga naye stori mbili tatu akinisifia kabla ya kubadilisha naye jezi. Aliniambia imi ni miongoni mwa wachezaji wazuri.
Alizungumza Sospeter Bajana kiungo wa klabu ya Azam FC.
Kiungo huyo wa klabu ya Azam FC ameongeza kuwa jambo hilo amelichukulia kwa ukubwa na amejifunza kitu kikubwa kwenye maisha yake ya soka lakini pia imemuongezea hali ya kujituma na kupambana ili aweze kufika juu zaidi ya alipo sasa.
Hakuwa na maneno mengi, lakini jambo aliloniambia ni; wewe ni kiungo mzuri sana, nilichukulia jambo lile thamani kubwa sana kwenye kazi yangu kupongezwa na mchezaji kama yule wa daraja la juu.
Sospeter Bajana aliongeza.
Mchezo huo wa kutafuta tiketi ya kufuzu fainali za kombe la Dunia ulimalizika kwa Taifa Stars kupoteza nyumbani katika Dimba la Benjamin Mkapa kwa jumla ya magoli 2-0 dhidi ya timu ya Taifa ya Morocco.
Sospeter Bajana huenda akakutana tena na Sofyan Amrabat mwezi January katika michuano ya Fainali za mataifa ya Afrika [AFCON2023] itakayofanyika nchini Ivory Coast kabla ya kukutana tena katika michuano hii ya kufuzu fainali za kombe la Dunia nchini Morocco. Tanzania ipo kundi F pamoja na timu ya Taifa ya Zambia, Congo DR na Morocco.
Hadi hivi sasa Tanzania ipo nafasi ya nne ya msimamo wa Kundi katika harakati za kutafuta tiketi ya kufuzu fainali za kombe la Dunia ikiwa na timu za Congo Brazzavile, Zambia, Morocco na Niger.