Wagosi wa Kaya kutoka Tanga, Coastal Union wamefanikiwa kupata ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji wao Tanzania Prisons kwenye mchezo wa ligi kuu ya NBC uliopigwa kwenye dimba la Sokoine, Mbeya na kufikisha alama 10 baada ya michezo 10 na kusogea hadi nafasi ya 10 ya msimamo wa ligi ya NBC.
Coastal Union walitangulia kupata goli na pekee dakika ya 17 kupitia kwa mchezaji wake raia wa Benin, Rolland Beakou akikwamisha kimiani mpira uliokuwa ukizagaazagaa langoni mwa Prisons baada ya mabeki wake kushindwa kuondoa mpira wa kona uliochongwa na Lucas Almeida Kikoti.
Mchezo uliendelea kuwa upande wa Coastal Union huku Prisons ikiwa kama timu ya pili wakiwa nyumbani. Walishindwa kuonyesha makali yao dakika 45 za kwanza na mpaka kwenda mapumziko, Coastal Union walikuwa kifua mbele kwa 1-0.
Kipindi cha pili kilirejea kwa kasi huku Tanzania Prisons wakionekana kuchangamka kutafuta goli la kusawazisha, Lakini Coastal walikuwa imara kulinda chao. Hata hivyo almanusura Coastal wapate goli la pili dakika ya 63 baada ya kazi nzuri ya Ibrahim Ajibu kushindwa kumaliziwa na Lucas Kikoti akiwa kwenye kisanduku baada ya kuingiliana na Greyson Gwalala.
Timu zote mbili zilifanya mabadiliko ya kinafasi na kimmfumo. Coastal wakimmpumzisha Ibrahimu Ajibu na kumuingiza Maabad Maabad kucheza kama mshambuliaji mmoja pekee huku Felly Mulumbu akichukua nafasi ya Lucas Kikoti ili kwenda kuongeza nguvu kwenye safu ya Ulinzi, wakati huo ambao Prisons wameongeza kasi ya ushambuliaji kwa Kumuingiza Beno Ngassa.
Mchezo uliendelea kuwa wa vuta nikuvute huku timu zote zikishambuliana kwa zamu. Licha ya mabadiliko ya kimmfumo, lakini bado Coastal walijaribu kufika golini kwa Prisons wakimmtumia Maabad, hata hivyo Prisons walikuwa imara huku wakijibu mashambulizi mara kadhaa lakini jitihada hazikuzaa matunda.
Dakika ya 93 kati ya dakika 4 zilizoongezwa kukamilisha dakika 90 za mchezo, Prisons walidhani wamepata goli la kusawazisha baada ya shuti kali la Salum Kimenya kwenda kugonga mwamba wa juu na kudunda kwenye mstari wagoli, kabla ya Beno kupaisha kwa kichwa wakati akijaribu kumalizia mpira huo.
Mpaka mpira unamalizika, Coastal Union wanapata ushindi wao wa 2 tu msimu huu baada ya michezo 10 na kufikisha alama 10. Prisons wakikubali kichapo cha pili mfululizo na kuendelea kujiweka pabaya kwenye msimamo wa ligi wakibaki na alama zao 7.