Connect with us

CAF Champions League

YANGA KUISHIKA HAPA BELOUIZDAD LEO

Young Africans wanatupa karata yao ya kwanza kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya takribani miaka 25 kupita tangu mwaka 1998, watakapomenyana na mabingwa watetezi wa ligi kuu nchini Algeria na wana robofainali mara tatu(3) mfululizo, CR Belouizdad.

CR Belouizdad wana kumbukumbu ya kucheza hatua ya makundi kwa mara 3 mtawalia huku Yanga ikiwa ni kitambo kidogo lakini sio suala la kuifanya Young Africans leo kuingia kinyonge.

Wakiwa na msimu bora wa mashindano ya vilabu ya CAF msimu uliopita wakifika Fainali ya Kombe la Shirikisho na kuukosa ubingwa kikanuni mbele ya USM Algier ya huko huko Algeria, Yanga imefanikiwa kujijengea heshima na kuonekana kuwa klabu ni tishio kwenye michuano hii. Belouizdad wataingia na tahadhari kubwa. Unaizungumzia Yanga ambayo ilikuwa miongoni mwa timu  zilizopata matokeo mazuri zaidi ugenini kwenye michuano ya CAF msimu uliopita, na hawana shida na uwanja wa Juillet 5.

Ukiachana tu na msimu bora waliokuwa nao, bado msimu huu Yanga inaonekana kuwa bora sana huku wakikiboresha zaidi kikosi chao wakiziba vilivyo baadhi ya mapengo ya kuondokewa na wachezaji wao muhimu kama Fiston Mayele, Feisal Salum, Yannick Bangala, Djuma Shaaban, Tuisila Kisinda na wengineo kwa muda mchache tu na kurejesha makali yao. Yanga imejipata sana hapa.

Kocha Marcos Paqueta anapenda sana ushindani na alishalisema hilo kueleka mchezo wa leo. Anafahamu Yanga ni timu ya aina gani na wana uwezo wa kufanya nini. Ni muumini mkubwa wa mfumo wa 4-4-2 Diamond au 4-3-3 huku akimmtumia zaidi Mamadou Samake kwenye kiungo na Leonel Wemba kwenye eneo la Ushambuliaji.

Mfumo wa mtaalamu Gamondi haupishani sana na wa Paqueta. Wote wanapenda kuwa na viungo wengi, mfumo wa 4-2-3-1 ni mfumo pendwa Gamondi na unakupa uwiano mzuri wa viungo wakati wa kushambulia na wakati wa kuzuia. Vita itakuwa kubwa sana eneo hili. Pacome Zouzoua, Maxi Mpia Nzengeli na Stephane Aziz Ki wamekuwa ndio wahimili wa mfumo huu hasa wakati wa kushambulia na Mudathir na Aucho wakiweka mizani sawa kwenye ukabaji.

Pamoja na yote hayo, Yanga wanapaswa kuingia kwenye mchezo huu wakijua kuwa Belouizdad hawahitaji matokeo yoyote leo zaidi ya ushindi, watatafuta kila aina ya nafasi ya kupata magoli na hasa hasa ya mapema ili kuwaondoa mchezoni na kuwafanya wajihisi wanyonge. Sina shaka na safu ya ulinzi ya Yanga, lakini haipaswi kuwa kazi ya safu ya ulinzi tu leo, kuzuia liwe jambo la timu nzima ili angalau kutoruhusu goli.

Sare ni matokeo mazuri pia kwa Yanga. Ni matokeo ambayo mchezo ukianza tu tayari yapo mikononi mwao ni wao tu kuyalinda kwanza huku wakitafuta ushindi taratibu. Yanga hawapaswi kuwa na papara za kutengeneza nafasi au kuufungua sana mchezo na kuruhusu kupishana nao, bali kulinda matokeo ya sare kwanza huku nafasi za kujaribu kupatikana alama 3 zikitengenezwa kwa kuwashinikiza kufanya makosa wakati wanajenga mashambulizi yaao.

Ikumbukwe hii ni hatua ya makundi na kila mtu anaringia kwake. Yanga tayari ana uzoefu nah ii hatu hata kama amecheza msimu mmoja tu hatua hii hivi karibuni lakini walahu wanajua wanapitia wapi kufuzu hatua hii. Wautumie huo uzoefu kuanzia mchezo wa leo, wasiamini sana kwenye rekodi za msimu uliopita kwani huu ni msimu mwingine na mashindano na mengine na pengine hata wapinzani ni wengine.

Makala Nyingine

More in CAF Champions League