JKT Tanzania na Ihefu zimetoshana nguvu leo kwenye mchezo wa ligi kuu ya NBC uliopigwa kwenye dimba la Azam Complex unaotumiwa na JKT Tanzania kama uwanja wao wa nyumbani kwa kutoka sare ya 1-1.
JKT Tanzania walitangulia kupata goli dakika ya 14 kupitia kwa Said Hamis Ndemla aliyemalizia kazi nzuri iliyofanywa na Sixtus Sabilo akitokea wingi ya kulia na kummpasia mfungaji aliyemalizia kwa utulivu mkubwa shuti kali lililommshinda golikipa Fikirini Bakari.
Dakika ya 16 yani dakika 2 tu baadae, Ihefu walisawazisha bao hilo kupitia kwa Ismail Mgunda likitokana na uzembe wa mabeki wakidhani kaotea wakati akipokea pasi murua na elekezi kutoka kwa kiungo fundi Shaaban Msala na yeye bila ajizi kumalizia kiustadi kabisa. 1-1 mpaka mapumziko.
Kipindi cha pili kilirejea kwa kasi huku walimu wote, Malale Hamsini na Moses Bassena wakifanya mabadiliko kwa nyakati tofauti ilipoonekana inafaa kwa mahitaji maalumu. Licha ya mvua kumwagika dakika kadhaa za mchezo lakini haikuondoa ladha ya soka tamu kutoka kwa timu hizi mbili.
Timu zote mbili zikitumia mfumo unaofanana wa 4-2-3-1 palikuwa na upinzania mkubwa hasa eneo la kiungo, Najimu Magulu, Hassan Nassoro wakibadilishana ujuzi na Shaaban Msala na Joseph Mahundi lakini bado ngome zote zilikuwa imara kwenye kujilinda pia.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika kwa kipyenga cha Ismail Mdoe, JKT Tanzania 1-1 Ihefu.
Baada ya mchezo kuisha, makocha wa timu zote mbili walikuwa na haya ya kusema
Hatujaridhika na matokeo kwakuwa tulikuwa uwanja wa nyumbani na tulitakiwa kupata alama zote tatu lakini kutotumia nafasi zetu kumesababisha kupata matokeo kama haya. Hili tatizo hata sijajua kwanini kwasababu tunaambiana kila siku mazoezini huwezi kujiita striker na hufungi karibu mechi ya 9 sasa. Hivyo tutaenda tena kulishughulikia hilo ili tujue tunafanyaje tufanye vizur zaidi michezo ijayo.
Malale Hamsini, Kocha Mkuu JKT Tanzania.
Tunashukuru kwa hii alama 1 ugenini lakini niseme ukweli timu yangu inaruhusu sana. Inafunga sawa lakini pia tunaruhusu. Kuna wachezaji wengi nawakosa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo majeruhi. Victor, Kunambi, Nyosso lakini ndio soka na hatuna namna. Tunakubali hii alama tutajipanga mchezo ujao tena.
Moses Bassena, Kocha Mkuu Ihefu.
Kwa matokeo hayo JKT Tanzania imebaki nafasi yake ya 7 wakifikisha alama 15 huku Ihefu wakipanda hadi nafasi ya 13 kutoka ya 14 wakifikisha alama 9.