Mwishoni mwa wiki iliyopita lilipigwa pambano kali lisilo la ubingwa kati ya bondia Mtanzania Abdallah Pazi [Dullah Mbabe] dhidi ya bondia kutoka nchini Congo DR, Eric Katompa. Pambano lililokuwa na mizunguko kumi [10] lilishuhudiwa mabondia wakimalizika mizunguko yote.
Pambano hilo lililazimika kuamulikwa kwa pointi ili kutambua bingwa wa pambano hilo ni nani na majaji wote watatu wakampa alama nyingi Eric katompa hivyo akatangazwa kuwa mshindi kwa mara ya pili mfululizo alizokutana na Abdallah Pazi. Eric alishinda kwa alama 93-97, 93-97, 92-98.
Baada ya pambano hilo bondia Abdallah Pazi hakufurahishwa na matokeo hayo ya majaji na pengine kuhisi ameonewa huku akinukuliwa akisema haelewi majaji na chama cha ngumi wanatatizo gani naye.
Sijui Majaji na Chama cha ngumi wana nia gani na mimi kwa kuwa nimecheza vizuri na mashabiki wameona kilichotokea.
Abdallah Pazi akizungumza baada ya pambano lake.
Bondia Ibrahim Class alikuwa sehemu ya watu waliokuwa upande wa Abdallah Pazi kwenye pambano hilo naye alionekana kusikitishwa na kilichotokea huku akiamini pengine kuna ugomvi upo baina ya Chama cha ngumi nchini na Abdallah pazi na kama upo akaomba wamsamehe ili maisha yaendelee lakini lengo kubwa akisisitiza pengine ungetolewa upendeleo kwa bondia wa nyumbani.
Baada ya kuzungumza maneno hayo ambayo mengi yaliripotiwa na dauda sports mapema leo amejitokeza hadharani na kuomba msamaha kwa chama cha ngumi nchini na kukiri kuwa alikosea kusema maneno hayo na kukielekezea chama cha ngumi badala yake alielekeza maneno hayo kwa majaji na marefa wa mchezo huo, huku akisema walistahili kutoa upendeleo kwa Abdallah Pazi.
Mimi nilikosea sio TPBRC, TPBRC hawana makosa ni chama cha marefa, lakini niseme tu nimeongea vile nimekosa, sikupaswa niongee vile mbele ya hadhara lakini tusameheane.
Ni kweli tumepoteza hilo halina shaka kwahiyo tutajipanga upya wakati mwingine unaokuja tutafanya vizuri.
Ibrahim Class bondia kutoka Tanzania akiomba msamaha kwa kauli yake aliyoitoa baada ya pambano la Abdallah Pazi.