Klabu ya soka ya Young Africans imepata matokeo ya sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya timu ya Al Ahly kwenye mchezo wa kundi D na kuzidi kujiweka kwenye mazingira magumu ya Kufuzu hatua inayofuata ya robo fainali.
Wakianza mchezo katika shinikizo la chini huku wakionekana kubadili umbo la kimchezo kutoka kwenye umbo lao la 4-2-3-1 hadi 5-3-2 au 3-5-2 kwa kuwepo na ingizo la Dickson Job kwenye safu ya Ulinzi kuliitoa Yanga kwenye falsafa yao ya kucheza mpira na kwa kiasi kikubwa kuiruhusu Al Ahly wamiliki mchezo hasa dakika 45 za kwanza.
Licha ya kwamba walicheza hivyo kutokana na kuwaheshimu wapinzani wao lakini Yanga ingeweza kuwa bora kiuchezaji. Ubaya ni kwamba mfumo huu ulimmlazimisha Maxi Nzengeli kushuka kama kiungo wa kati pamoja na Pacome Zouzoua na Aucho huku Azizi Ki na Mzize wakicheza kama 9 na 10 tofauti na ilivyozoeleka wakicheza kutokea pembeni kwasababu tayari Yao Kouassi na Lomalisa Mutambala walikuwa wakicheza kupitia pembe hizi mbili. Yanga ni kama walijifunga kati kati ya uwanja.
Kipindi cha pili timu zote zilikuja na mabadiliko kiuchezaji huku Al Ahly wakifanya mabadiliko kuendana na mfumo wa Yanga ili watoshane kwenye viungo. Kumuingiza Afsha na kumtoa Emam Ashour huku wakijizatiti kwa Kumuingiza Fouad Karim nafasi ya Hassan El Shahat huku Viungo Amr Solia na Mohamed Taher wakichukua nafasi za Mshambuliaji Kahraba na Kiungo Marwan Ataya.
Mchezo ulienda mpaka dakika ya 76 huku Al Ahly wakionekana kuutaka zaidi mchezo wakishambulia kwa kasi mpya iliyopia lakini pia ulinzi ukiimarika kwa kuongeza Fouad Karim. Yanga walielemewa hasa eneo la kiungo na kuamua kuwapumzisha Clement Mzize na kumuingiza Kennedy Musonda huku akimtoa pia Maxi Nzengeli ambaye hakuwa na wakati mzuri na kuamua kuongeza nguvu kwenye kiungo cha kukaba kwa kumuingiza Zawadi Mauya.
Dakika ya 86 Percy Tau aliwapatia bao la Kuongoza timu ya Al Ahly kabla ya Pacome Zouzoua kuisawazishia Yanga dakika ya 90+1 akimalizia kazi nzuri aliyoianzisha yeye mwenyewe akicheza one-two safi na Kennedy Musonda.
Kwa matokeo haya Yanga anafikisha alama 1 na ana kibaru kingine kigumu ugenini dhdi ya Medeama kwenye mchezo utakaopigwa nchini Ghana Tarehe 08 Disemba,2023. Yanga ni lazima washinde walahu michezo mitatu kati ya 4 iliyosalia ili kufufua matuamaini ya kufuzu hatua ya robo fainali.