Wakati Jumanne Elfadhil anaipa Tanzania Prisons alama 3 muhimu mbele ya Dodoma Jiji kwenye uwanja wao wa nyumbani Sokoine, Ihefu walikabwa koo na JKT Tanzania kwa sare 1-1 huku bao lao la kusawazisha likifungwa na Ismail Mgunda dakika 2 tu tangu Said Ndemla aitangulize JKT.
Leo wamba hawa wawili wanakutana huko Highland Estates, Mbarali. Ihefu wakiikaribisha Tanzania Prisons kwenye mchezo wa ligi kuu NBC huku wote wakiwa kwenye nafasi 4 za chini za aidha kushuka daraja au kucheza play off. Mechi hii inatarajiwa kuwa ya kukata na shoka kutokana na mahitaji yaliyopo mezani.
Ihefu wapo nafasi ya 14 wakiwa na alama 9 tu baada ya mechi 11 huku Tanzania Prisons wakiwa nafasi ya 13 wakiwa na alama 10 baada ya michezo yao 11 pia huku wote wakitazama kutoka kwenye eneo hilo la hatari na walahu kuingia kwenye nafasi 10 za juu. Moto!
Furaha kubwa kwa Ihefu ni kurejea kwa baadhi ya nyota wao muhimu kikosini kama Juma Nyosso, Issa Rashid, Raphael Daud Loth, Victor Akpan na wengine ambao Mwalimu Bassena alikiri kuwa kuwakosa nyota hao kumechangia kwa kiasi kikubwa timu yake kutofanya vizuri kwenye michezo ya hivi karibuni huku akilia zaidi na safu yake ya ushambuliaji lakini kurejea pia kwa Charles Ilanfya kunamuongezea wigo wa kuchagua.
Huwezi kuchukua lolote kutoka kwa Prisons kwenye mchezo huu kwani licha ya kuwa na nyakati za panda shuka lakini safu yao ya ushambuliaji haiko vibaya sana kwani ukiwaacha wakongwe kama Samson Mbangula na Jeremiah Mgunda, vijana Beno Ngassa, Edwin Balua na Zabona Mayombya ni wa moto na hawatabiriki. Sio wa kubezwa hata kidogo.
Mchezo utapigwa majira ya saa 10 jioni hii leo.