Connect with us

Timu za Taifa za Wanawake za Tanzania

TWIGA STARS KIBARUANI TOGO LEO.

Timu ya Taifa ya wanawake ya Tanzania “Twiga Stars” inatarajiwa kushuka dimbani hii leo majira ya saa moja jioni [19:00] kuikabili timu ya Taifa ya wanawake ya Togo katika mchezo wa pili wa kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa wanawake.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa katika uwanja wa Kegue uliopo katika Jiji la Lome nchini Togo. Uwanja huo unauwezo wa kubeba watazamaji 25,000 ukiwa umeanzishwa mwaka 2000.

Kuelekea katika mchezo huo timu ya Taifa ya wanawake ya Tanzania inafaida ya kuwa na magoli matatu [3] waliyoyapata katika mchezo wa kwanza uliopigwa katika uwanja wa Azam Complex, Dar Es Salaam.

Magoli ya Tanzanite yalifungwa na Opah Clement aliyefunga mawili [2] na Yawa Konou aliyejifunga.

Mchezaji wa Twiga Stars Fatma Issa amesema kwa upande wao kama wachezaji wamejiandaa kufanya vizuri katika mchezo wao wa leo.

Sisi kama wachezaji tumejiandaa vizuri kuelekea mchezo wetu wa leo, natumai tutafanya vizuri.

Fatma Issa, Mchezaji Twiga Stars

Kwa upande wa nyota mwingine wa Twiga Stars Stumai Abdallah amesema mazingira ya Togo ni kama ilivyo kwa Tanzania tu hayana tofauti sana na wamejiandaa vyema na mchezo wa leo.

Uwanja upo vizuri kama Tanzania tu, tutapambana ili tupate matokeo mazuri tuweze kwenda WAFCON.

Stumai Abdallah, mchezaji wa Twiga Stars.

Kocha mkuu wa kikosi cha Twiga Stars Bakari shime amesema maandalizi ya mchezo wa leo yalifanyika kabla ya mchezo wa kwanza.

Maandalizi yote kwaajili ya mchezo wetu dhidi ya Togo yameshakamilika zamani kabla ya mchezo wa kwanza.

Lazima tutafute njia nzuri ya kuzuia ili kuwasoma wapinzani wetu wanacheza vipi wakiwa nyumbani ili mwisho wa siku tupate matokeo yatakayotupeleka WAFCON.

Bakari Shime, Kocha mkuu Twiga Stars.

Twiga stars inahitaji kupata matokeo hii leo ili ijihakikishie nafasi ya kufuzu fainali za mataifa ya Afrika zitakazofanyika nchini Morocco.

Makala Nyingine

More in Timu za Taifa za Wanawake za Tanzania