Klabu ya Simba imesafiri hadi nchini Morocco kwaajili ya mchezo wake wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi ya Wydad AC utakaopigwa katika Jiji la Marrakech nchini Morocco.
Huu utakuwa ni mchezo wa tatu [3] kwa Simba kucheza katika hatua hii ya makundi, baada ya kucheza michezo miwili ya mwanzo na kuambulia alama moja pekee.
Utakuwa ni wasaa kwa Simba kutafuta alama tatu za kwanza mbele ya timu ambayo haijapata alama yoyote kutoka kwenye michezo miwili ambayo imecheza.
Kutoka nchini Morocco Afisa habari wa klabu ya Simba Ahmed Ally ameweka wazi kuwa hakuna mchezaji mwenye majeraha na wameizoea hali ya hewa kwahivyo wapo tayari kwa mchezo wa Jumamosi hii.
Hakuna mchezaji aliye na majeraha wote tupo vizuri.
Ahmed ally, Afisa habari wa Simba.
Kuhusu kufanyiwa figisu kama ambavyo klabu nyingi zimekuwa zikiripoti pindi zinapotembelea Afrika Kaskazini amesema kwasasa Simba inaogopwa sana hivyo hakuna wa kuifanyia figisu.
Simba ni timu kubwa Barani Afrika kila mtu anatuogopa hakuna atakayethubutu kutuletea mizengwe.
Ahmed, Aliongeza.
Hali ya hewa tumeizoea na tulikuwa tumeshajiandaa na ndio maana tumekuja mapema huku.
Benchikha anawaambia vijana wake wasibweteke kutokana na matokeo tuliyoyapata dhidi ya Jwaneng Galaxy.
Ahmed Amesema.
Awali mchezo wa Simba na Wydad AC ulipaswa kuchezwa katika uwanja wa Mohamed V katika Jiji la Casablanca lakini uwanja huo upo kwenye marekebisho hivyo mchezo huo utachezwa katika uwanja wa Marrakech uliopo kwenye Jiji la Marrakech nchini Morocco.
Young Africans pia ina kibarua Ijumaa hii cha kuikabili Medeama ambayo imekuwa na wakati mzuri katika michezo yake ya nyumbani kimataifa katika uwanja wa Baba Yara uliopo Kumasi nchini Ghana.
Kuelekea katika mchezo huo Daktari wa klabu ya Yanga Moses Etutu amesema kikosi chake kipo salama isipokuwa Jonas Mkude ambaye alipata changamoto baada ya kutumia chakula.
Mwenzetu mmoja [Jonas Mkude] alipata allegy kidogo baada ya kula chakula, wachezaji wengine wapo vizuri hadi hivi sasa.
Moses Etutu – Daktari wa Yanga.
Yanga nayo pia inasaka alama tatu za kwanza baada ya kushindwa kuzipata katika michezo miwili iliyopita ikiambulia alama moja pekee baada ya kutoka sare mchezo mmoja na kupoteza mchezo mmoja.
Medeama imepata alama tatu katika mchezo dhidi ya CR Belouizdad na kupoteza mchezo mmoja mbele ya Al Ahly.
Dauda Sports inazitakia kila lakheri klabu zetu zote mbili zinazoiwakilisha nchi na ukanda wa CECAFA katika michuano hii mikubwa Barani Afrika.