Connect with us

NBC Premier League

TATIZO MOTISHA MASHUJAA KUFANYA VIBAYA.

Mwenyekiti wa klabu ya Mashujaa inayoshiriki Ligi kuu kandanda Tanzania Bara Meja Yahya Mgaya ameeleza chanzo cha timu hiyo kutokufanya vizuri kwenye msimu wake wa kwanza wa Ligi kuu ni pamoja na kutokuwa na hamasa ya kutosha kutoka kwa wadau mbalimbali wa mkoa huo kama ambavyo walikuwa wanafanya wakati timu hiyo ikiwa championship.

Timu zetu za mikoani asikudanganye mtu, huwezi kushinda bila hamasa, tuliunda kamati ya hamasa na kuwapa wachezaji bonus ili kuhakikisha timu ina panda daraja msimu huu.

Kwenye hali ambayo tupo sasa hivi, tumekosa hamasa kutoka kwa wadau mbalimbali.

Meja Yahya Mgaya amesema.

Taarifa mbalimbali zilikuwa zikieleza kuwa miongoni mwa sababu zinazoifanya Mashujaa kutokufanya vizuri hivi karibuni ni kuchelewesha malipo ya mishahara kwa wachezaji wake jambo ambalo mwenyekiti amesema sio kweli.

Katika timu ambazo zinalipa vizuri, timu yetu inalipa vizuri na kwa wakati, na kuna bonus kila mechi kwa wachezaji, timu ikishinda inawekewa mzigo wake mezani.

Yahya Aliongeza.

Aidha Mwenyekiti ameeleza kuwa klabu hiyo inajipanga kufanya usajili wa maana katika dirisha dogo la usajili kwa maingizo ya nyota ambao watainusuru timu hiyo kutoka kwenye nafasi ilipo timu hiyo kwasasa.

Dirisha dogo kutokana na mapendekezo ya mwalimu tutaongeza wachezaji wa maana ambao watatuletea matokeo na kutunusuru kwenye nafasi tuliyopo na sio wa majaribio.

Kwa uwezo wa taasisi yetu na timu yetu, tunauwezo wa kuchukua mchezaji wa gharama yoyote atakayekuja kutubadilishia matokeo, hatuchukui pancha sasa hivi.

Meja Yahya Mgaya amesema.

Mashujaa imepoteza michezo minne mfululizo na kuambulia sare katika mchezo mmoja kati ya michezo mitano [5] iliyopita.

Katika mchezo dhidi ya Tabora United waliotoka sare ya kufungana goli 1-1 mashabiki uwanjani walikuwa wanaimba nyimbo za kutokumhitaji kocha wa kikosi hicho Abdallah Bares.

Mwenyekiti wa klabu hiyo Mgaya amesema wamekisikia kile ambacho mashabiki wana kilalamikia na tayari wameongea na mwalimu kumweleza kuwa wana Kigoma wanachotaka ni ushindi tu.

Walichokiimba mashabiki uwanjani kuhusu kutokumtaka kocha sisi tunakisikia na mwalimu amekiona, Tumemwambia mwalimu wana Kigoma na sisi tunachotaka ni matokeo na ameshaanza kulifanyia kazi mazoezini.

Meja Yahya alimalizia.

Mashujaa leo tena itakuwa na kibarua mbele ya Tanzania Prison katika uwanja wa CCM Lake Tanganyika mkoani Kigoma majira ya saa 10:00 Jioni, mashabiki wakitumaini baada ya kufikisha ujumbe wao utafanyiwa kazi.

Kwasasa mashujaa ipo nafasi ya 15 kati ya timu 16 zinazoshiriki Ligi kuu kandanda Tanzania Bara, inahitaji Juhudi za dhati ili kuhakikisha inasalia Ligi kuu msimu ujao

Makala Nyingine

More in NBC Premier League