Connect with us

Makala Nyingine

AZAM FC HAIKAMATIKI, YAINYUKA JKT

Azam FC wamefanikiwa kupata ushindi wao wa 5 mfululizo na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi kuu Tanzania bara baada ya kuwanyuka JKT Tanzania kwa mabao 2-1 na kufikisha alama 28.

Azam walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Sospeter Bajana dakika ya kwanza tu ya mchezo kwa Shuti kali lililomshinda golikipa Ismail Salehe.

Waliendelea kuutawala mchezo huku wakitengeneza nafasi kadhaa za kufunga, Prince Dube alipata nafasi ya kuipatia Azam goli la pili lakini mpira wake wa kichwa ulipanguliwa vema na Ismail Salehe. Kona haikuzaa matunda.

Azama FC walidhani wamepata penati dakika ya 27 ya mchezo baada mchezaji wao Lusajo Mwaikenda kufanyiwa madhambi na Edson Katanga lakini mwamuzi Heri Sasii alikuwa na mawazo tofauti.

Wakiwa wameamini kuwa wameushika mchezo, JKT Tanzania wakawashitukiza kwa shambulizi moja tu la hatari, golikipa Ahamada akiwa kwenye harakati za kuokoa mpira uliokuwa unaelelezwa kwa Hassan Kapalata, ulidondoka vizuri kwa mfungaji Najim Magulu aliyepiga shuti lilotinga nyavuni pakiwa hakuna golikipa. Dakika ya 37 ikawa 1-1.

Timu zote zilienda mapumziko kwa sare ya 1-1.

Dakika 45 za kipindi cha pili zilirejea pakiwa na nidhamu ya hali ya juu. Huku JKT wakicheza chini sana na kuwashambulia Azam kwa nyakati. Wakiwa hawajafanya badiliko lolote, Kocha Malale Hamsini ni kama aliridhika na mpango kazi wake.

Baada ya kufanya mashambulizi mengi kwa muda mrefu bila mafanikio mwalimu Dabo aliamua kufanya mabadiliko kadhaa kwenye mfumo wake wa uchezaji baada ya kumuingiza Iddy Nado na Abdul Sopu kwenye safu ya ushambuliaji ikimaanisha Dube na Kipre wanacheza kama washambuliaji wawili huku Sopu na Iddy wakicheza kama mawinga kwenye 4-4-2.

Dakika ya 84 ya mchezo, Iddy Selemani “Nado” alifanya anachokifanyaga bora siku zote akiingiaga kutoka benchi akiwapatia Azam bao la pili na la ushindi akimalizia kazi nzuri ya Kipre Jr. Akitokea pembeni.

Licha ya Mwalimu Malale kufanya mabadiliko kadhaa kwenye safu yake ya ushambuliaji akimuingiza, Edward Songo, Selembe pamoja na Ismail Aziz Kader bado JKT Tanzania haikuweza kufua dafu.

Mpaka dakika ya 90 ya mchezo, Azam FC 2-1 JKT Tanzania.

Makala Nyingine

More in Makala Nyingine