Singida FG walionyesha kweli wako nyumbani wakicheza vizuri wakionana na kujiamini sana huku wakiwa timu bora zaidi kwenye kipindi cha kwanza.
Nafasi hazikuwa nyingi kipindi hiki hata hivyo huku KMC wakipiga shuti 1 pekee lililolenga lango kutoka kwa Fredy Tangalo hata hivyo shuti lake lilikuwa dhaifu kwa golikipa Parapanda.
Singida FG walionekana kukosana nafasi nyingi za wazi zaidi kupitia kwa Habibu Kyombo ambaye mashuti yake mawili mfululizo yalipanguliwa vema na Wilbol Maseke. Haikuwa siku nzuri kwa Marouf Tchakei kwenye dakika hizi za mchezo, mipira yake iliyokufa mingi ikikosa macho.
Hapakuwa na mengi ya kuripoti kipindi cha kwanza kwani kilienda bubu hadi mapumziko japo utasifu pia utulivu wa KMC kwenye safu ya ulinzi na eneo la kiungo. Issah Ndala na Kenny Ally Mwambungu wakileta uhai hii leo.
Kipindi cha pili kilirudi tena na kasi huku timu mwenyeji wakiendelea kuonyesha kiu ya kutafuta matokeo hii leo. Lakini hata hivyo dakika 15 za mwanzo bado milango ilikuwa migumu.
KMC walianza kurudi kwenye mchezo huku wakiharibu kupanga vizuri mashambulizi yao lakini walinzi wa Singida FG wakiongozwa na Biermes Carno walionekana kuwa makini kuwazuia.
Mchezo ni kama ulikuwa kwenye mzani sawa huku kila timu ikimsikilizia mpinzani wake. Pakiwa na matumizi mengi ya akili na nidhamu, mchezo ulimalizika kwa suluhu ya 0-0 na timu zote kujinyakulia alama 1.
Kwa matokeo haya Singida FG wanasogea nafasi ya 3 na KMC wanasogea nafasi ya 4 wote wakifikisha alama 20 wakimshusha Simba SC wakiwa na alama zao 19 baada ya michezo 8.