Connect with us

Makala Nyingine

WANANCHI WAITAFUNA MIWA YA MTIBWA

Mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara, Yanga, leo wamewafumua Mtibwa Sugar kwa mabao 4-1 na kufikisha alama 27 baada ya michezo 10 na kuendelea kusalia nafasi yao ya 2 nyuma ya Azam.

Kama ilivyotarajiwa na wengi, Yanga walianza mchezo kwa kuumiliki mpira kwa kiasi kikubwa huku wakikishambulia lango la Mtibwa mfululizo lakini Washambuliaji Clement Mzize, Jesus Moloko na Skudu Makudubela walikosa utulivu wa kuzitumia nafasi hizo.

Mtibwa Sugar walionekana kuwa wenye nidhamu pia muda mwingi wa mchezo huku wakijibu Mashambulizi kwa kushtukiza kupitia Kwa Juma Nyangi, Kassim Haruna, Ladack Chasambi na Matheo Anthony lakini majaribio yao muda mwingi hayakumpa wakati mgumu Djigui Diarra.

Pengine isingekuwa uhodari wa Mohammed Makaka, Mtibwa wangekuwa tayari wako nyuma ndani ya dakia 30 za mwanzo, akiokoa mashuti makali ya Maxi Nzengeli na Clement Mzize. Mtibwa walionyesha kungamara dakika hizi na kuufanya mchezo kuonekana mgumu huku ikihitaji Yanga kuongeza kasi ya mchezo.

Dakika ya 46+ ndani ya dakika za nyongeza kukamilisha dakika 45 za kipindi cha kwanza, Clement Mzize alifanyiwa madhambi kwenye eneo la penati na Nahodha Oscar Masai na muamuzi kuamuru upigwe mkwaju wa penati uliofungwa vizuri kabisa na Stephane Aziz Ki.

Mpaka mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0

Yanga walirudi kipindi cha pili wakiwa na kasi lakini Mtibwa nao waliendelea kuwa imara. Yanga walifanya mabadiliko na kuwaingiza Musonda, Pacome na Farid. Mabadiliko haya yaliongezea msukumo wa mashambulizi kwa upande wao na kuwafanya Mtibwa waanze kupoa.

Dakika 70 Stephane Azizi Ki aliiandikia Yanga bao la 2 na la kwake la 2 kwa siku baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Kibwana Shomari, akampiga “tobo” Oscar Masai kabla ya kuudokoa mpira uliomshinda Makaka.

Mtibwa waliendelea kuelemewa na Yanga kuzidisha presha kwao na dakika ya 76 ya mchezo, Kennedy Musonda alipokea pasi ya kichwa kutoka kwa Jesus Moloko na yeye kupiga shuti kwa mtindo ‘semi voley’ lililomuacha Makaka asiwe na la kufanya. Yanga 3-0 Mtibwa.

Wakati Mtibwa wakiendelea kujiuliza nini kimewapiga, huku wakiendelea kutawaliwa kimchezo, Mahlatse “Skudu” Makudubela aliwainua tena Wananchi kwa shangwe baada ya kufunga bao la 4 kwa timu yake dakika ya 86. Goli lake la kwanza msimu huu kwenye dakika zake 90 za kwanza kabisa msimu huu pia.

Dakika ya 90 ya mchezo, Seif Rashid Karihe aliifungia Mtibwa Sugar bao kwa shuti la mbali wakati wachezaji wa Yanga wakidhani mwenzao Ibrahim Bacca amefanyiwa madhambi na yeye kumuona Djigui Diarra ametokea na kupiga shuti lililoenda moja kwa moja nyavuni.

Hata hivyo goli hilo lilikuwa ni la kufutia machozi tu kwani mpaka filimbi ya mwisho ya Muamuzi, Yanga walibuka washindi na kujikusanyia alama 3 muhimu huku vijana wa Zubery Katwila wakiendelea kuwa kwenye hali mbaya msimu huu.

Makala Nyingine

More in Makala Nyingine