Connect with us

CAF Champions League

SIMBA YAIWASHIA MOTO WYDAD KWA MKAPA

Simba Sports Club wameonyesha umwamba wao kwenye michuano hii ya ligi ya Mabingwa Afrika huku wakienda na kauli mbiu yao ya “Haijaisha Mpaka Imeisha” kwa kuwachapa Wydad AC kwa jumla ya mabao 2-0 kwenye mchezo wa kundi B uliopigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa.

Simba walionyesha utulivu mkubwa kwenye mchezo wenye presha na kuhakikisha hawawapi nafasi kubwa Wydad kuwatawala kimchezo huku pakionekana pengo kubwa kwenye eneo la kiungo upande wa Wydad wakimkosa nahodha wao Yahya Jabrane.

Mifumo ikionekana kuwa tofauti leo kwa timu zote kimmkakati, Simba wakicheza 4-4-2 huku Essomba Onana na Jean Baleke wakicheza kama washambuliaji wawili wa juu huku Wydad wakicheza kwenye umbo la 4-3-3.

Dakika ya 36 mfumo ulionekana kumlipa Kocha Benchikha kwa Simba kupeleka mashinikizo mengi langoni mwa Wydad, pasi tamu ya kutengewa kutoka kwa Kibu Denis kwenda kwa Essomba Onana ambaye naye anapiga shuti kali la chini chini na kuitanguliza Simba. 1-0 kwa Simba.

Wakati Wydad wakiduwazwa na goli hilo, Essomba Onana akawainua tena Wana Simba baada ya kupachika bao la pili kwake na kwa timu yake ya Simba baada ya kugongeana vizuri na Mzamiru Yassin kisha yeye bila ajizi kupasia tu nyavuni goli tamu kabisa na Simba kuwa mbele kwa bao 2-0 dakika ya 38.

Kipindi hiki cha kwanza hutoacha kusifu uhodari wa golikipa Ayoub Lakred ambaye aliokoa mashambulizi mengi ya Hatari kutoka kwa Bouly Sambou na Zacharia Badroui.

Mpaka mapumziko Simba walikuwa mbele kwa mabao 2-0.

Wydad walirudi kipindi cha pili na mkakati kabambe wa kutaka kusawazisha mabao hayo lakini Benchikha alikuwa na “sapraizi” yake pia.

Jean Othos Baleke alikosa nafasi ya wazi kuiandikia Simba bao la 3 dakika ya 55 akipokea pasi murua kutoka kwa Shomari Kapombe Lakini shuti lake lilikuwa hafifu akiwa karibu kabisa na goli

Dakika ya 62, Kibu Denis aliachia shuti kali nje kidogo ya eneo la 18 la Wydad lakini Golikipa Yousouff El Motie alikuwa sambamba nalo.

Wakati Wydad wakiwa wanasukuma mashambulizi mfululizo, Benchikha aliamua kufanya mabadiliko ili kulinda alichokipata kwa kuwatoa Essomba Onana, Kibu Denis, Clatous Chama kwenye eneo la ushambuliaji na kuwaingiza John Bocco huku Israh Mwenda na David Kameta Duchu wakienda kufanya majukumu ya Ulinzi.

Mchezo ukiwa unaendelea, Wydad walizidi kuwa huru kucheza na kujenga mashambulizi kwakuwa Simba walikuwa wakichezea chini sana. Kuimarisha Ulinzi, Benchikha akamtoa Jean Baleke na Mzamiru Yassini na kuwaingiza Hamisi Abdallah Kwenye Kiungo na Kennedy Juma kwenda kuimarisha safu ya Ulinzi ukionekana mfumo wa 5-4-1. John Bocco akiwa Mshambuliaji pekee.

Nidhamu kubwa ya Ulinzi iliweza kuwasaidia Simba kulinda ushindi wao. Wakicheza kwa kufuata maelekezo waliweza kuwafanya Wydad wasiwe na mashambulizi ya hatari huku pia walinzi wakisaidiana golikipa wao Lakred waliweza kuokoa baadhi ya mipira hatari.

Mpaka dakika 90 zinatamatika, Simba waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 ushindi ambao unawasogeza mpaka nafasi ya 2 kwenye msimamo nyuma ya ASEC Mimosas wakiwa na alama 5.

Makala Nyingine

More in CAF Champions League