Azam FC wameendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi kuu ya soka Tanzania Bara baada ya kuwagaragaza Kagera Sugar kwa mabao 4-0 kwenye mchezo uliochezwa kwenye dimba la Kaitaba, Kagera na kufikisha alama 31 baada ya michezo yao 13.
Azam walianza mchezo kwa nguvu mapema tu na haikuwachukua muda kuandika bao lao la kwanza kupitia kwa Feisal Salum dakika ya 9 tu akiachia shuti kali nje kidogo ya eneo la 18 la timu ya Kagera Sugar, mpira uliomshinda Ramadhani Chalamanda.
Haikuwachukua muda matajiri hawa wa Chamazi kuandika bao la pili kupitia kwa ‘mwanafalme’, Prince Dube akimalizia kazi nzuri iliyoanzishwa na Feisal Salum akipeleka pasi kulia alipo Kipre Jr kabla ya yeye kumpa pasi elekezi muuaji anauetabasamu ambaye hakufanya ajizi. 2-0 Azam dakika ya 11 tu ya mchezo.
Kagera Sugar ni kama walionekana kuvurugika hasa eneo la katikati ya uwanja, James Akaminko na Yahya Zaid wakitamba vilivyo mbele ya Hijja Shamte na Abdallah Seseme ambao walionekana kukosa muunganiko mzuri.
Wakitumia mfumo wa 4-2-3-1, Obrey Chirwa alikuwa mnyonge akikosa huduma za maana kutoka kwa Cleophace Mkandala, Ally Nassoro Ufudu na Kasozi kwakuwa viungo wakabaji wa chini walizidiwa hivyo muda mwingi iliwalizimu kushuka kusaidia.
Pembezoni mwa Uwanja kulifanya Azam wawe huru kwakuwa Kagera walikuwa wamejaa katikati, David Luhende na Dickson Mhilu walikuwa na mzigo mkubwa sana kuwadhibiti Pascal Msindo na Lusajo Mwaikenda ambao walikuwa kwenye kiwango bora sana.
Kuthibitisha hilo, dakika ya 45 ya mchezo, Pascal Mshindo alishindilia msumari wa 3 akimalizia shambulizi zuri lililoanzishwa na Feisal Salum tena, aliyepiga pasi mnyunyizi kwa Prince Dube ambaye naye bila uchoyo akamtengenezea mfungaji kwa Kichwa na Pascal Mshindo akamalizia kwa mguu wake wa kulia.
Ni Azam wakaenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar ikiyokuwa dhohofu kabisa.
Hakuna jipya la maana walilorejea nalo Kagera Sugar kipindi cha pili. Bado walionekana ni timu ya pili kiwanjani huku wakionekana kutokuwa na mipango ya maana kupata goli.
Dakika ya 51, Kagera Sugar walipata penati pengine ya kuwarudisha mchezoni lakini bwana mdogo Zubery Foba akaibuka shujaa kwa Azam mbele ya mchezaji wa zamani wa Azam, Obrey Chirwa kwa kupangua mkwaju wake wa penati. Mioyo ya wana Super Nkurukumbi ikaendelea kukosa matumaini.
Azam FC walirejea tena kwenye siti mbele, wakiwa watulivu kwenye kila eneo la kiwanja. Wakigongeana pasi na mikakati ikionekana.
Aliassane Diao aliyeingia kipindi cha pili, alihitimisha karamu ya mabao baada ya kutupia kimiani goli la 4 kwa upande wa Azam dakika ya 84 ya mchezo na kuwaacha Kagera Sugar wakizidi kutota kabisa.
Dakika 90 zikamalizika kwa Azam FC kushinda kwa jumla ya mabao 4-0.