Connect with us

NBC Premier League

GEITA GOLD YAIZIMA SINGIDA FG

Goli la dakika ya 72 la Valentino Mashaka lilitosha kuwapa ushindi muhimu Geita Gold dhidi ya Singida Fountain Gate kwenye mchezo wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara uliopigwa kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari ya wasichana ya Nyankumbu.

Geita Gold walionyesha njaa ya kutaka matokeo mapema tu kwenye mchezo wakicheza kimkakati huku wakisukuma mashambulizi kwa wapinzani wao.

Singida FG hawakuonekana kuwa kwenye ubora wao leo kwani licha pia ya kutengeneza nafasi hawakuweza kuwa wafanisi kwenye kuzitumia.

Akitokea Benchi, Valentino Mashaka aliongeza kasi ya mashambulizi upande wa Geita Gold akishirikiana vema na safu ya kiungo ambayo ilikuwa kwenye ubora sana hii leo. Edmund John na Tariq Kiakala waliwapa wakati mgumu Biemes Carno na kampani yake.

Dakika ya 72, uzembe wa walinzi kushindwa kumkaba Valentino Mashaka wakati Krosi murua ya Samuel Onditi ikipigwa ulimpa nafasi ya kupiga kichwa mchumio kilichomshinda golikipa Parapanda.

Ni kama mchezo ulikuwa umeisha kuanzia hapo, Geita wakizidisha nidhamu kubwa kwenye kulinda walichonacho kwenye dakika ambazo Singida FG walicharuka kutaka kusawazisha.

Dakika zote 90 zikamalizika na kuhalalisha alama 3 zote kwenye kwa wenyeji Geita Gold kwa ushindi wa bao 1-0. Ushindi huu unawasogeza Geita Gold mpaka nafasi ya 10 wakifikisha alama 16 huku Singida FG wakisalia na alama zao 20 nafasi ya 4.

Makala Nyingine

More in NBC Premier League