Connect with us

NBC Premier League

PRISONS YAWATAMBIA NAMUNGO SOKOINE

Tanzania Prisons wamevuna alama 3 muhimu nyumbani kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuwafunga Namungo kwa bao 1-0 kwenye mchezo uliopigwa kwenye dimba la Sokoine, jijini Mbeya.

Tanzania Prisons walicheza kitofauti kwenye mchezo wa leo sio tu matumizi makubwa ya nguvu bali pia ufundi na mikimbio ya kutengeneza nafasi nyuma ya mabeki wa Namungo.

Japokuwa wote walikuwa kwenye mfumo wa 4-4-2 lakini Prisons walkonekan kufaidika zaidi na Mawinga wake, Edwin Balua na Zabona Mayombya kwenye kuwatengenezea nafasi washambuliaji wake wawili, Samson Mbangula na Jeremiah Juma.

Aidha upande wa Namungo hapakuwa na muunganiko mzuri sana kutoka kwenye kiungo cha juu kuelekea kwenye pembe zao alikokuwa akicheza Hashim Manyanya na Jacob Massawe ambapo leo Erasto Nyoni alikuwa akicheza kama Namba 8 nyuma ya Pius Buswita na Reliants Lusajo.

Dakika ya 42 ya mchezo, Samson Mbangula aliwatanguliza wenyeji kwa kufunga bao ikiwa dakika chache tu kuelekea mapumziko.

Kipindi cha pili kikirejea kwa utulivu kwa timu zote mbili japo Namungo walikuja na mpanga wa kutaka kusawazisha bao na kuwafanya Prisons kuanza kuwa makini kiulinzi.

Yona Amos aliokoa shuti kali la Pius Buswita dakika ya 48 tu baada ya walinzi kufanya uzembe wa kuchelewa kufika kummdhibiti.

Prisons walijibu shambulizi kupitia kwa Edwin Balua ambaye alikuwa na nafasi ya wazi kabisa kuiandikia timu yake bao la pili lakini alikosa utulivu na mpira wake kwenda nje ya lango bila kumsumbua Jonathan Nahimana.

Nahimana aliendelea kusakamwa langoni mwake ikimlazimu kufanya kazi ya ziada kuokoa michomo ya washambuliaji wa Prisons. Shuti kali la Samson Mbangula dakika ya 68, alilipangua vema huku kona iliyotokana haikuzaa matunda. Prisons walimuingiza Joshua Nyantini nafasi ya Jeremiah Juma dakika hizi pia. Lakini Namungo waliamua kumtoa Erasto Nyoni na kumuingiza James Mwashinga eneo la kiungo dakika ya 74.

timu zote mbili ziliendeleana kushambuliana kwa zamu, Namungo wakitaka kusawazisha lakini Prisons wakiona nafasi ya kuongeza Uongozi wao. Lakini mpaka filimbi ya mwisho ya muamuzi Liston Hiari inapulizwa, Tanzania Prisons waliibuka kidedea kwa ushindi wa bao 1-0.

Kwa matokeo hayo Prisons wanasogea mpaka nafasi ya 9 wakifikisha alama 17 nyuma ya Namungo wenyewe wenye alama 17 lakini wakipishana kwa tofauti ya magoli.

Makala Nyingine

More in NBC Premier League