Yanga walipata bao la kuongoza kupitia kwa Willyson Christopher dakika ya 16 ya mchezo akiachia shuti kali ndani ya eneo la penati la Simba, licha ya jitihada za golikipa kujaribu kupangua lakini mpira ulimzidi nguvu na kuingia kimiani.
Simba hawakuonekana kuwa bora hasa kwenye kipindi cha kwanza huku Yanga wakiumiliki mpira kwa muda mwingi wakipigiana pasi fupi fupi na za haraka pia hususani kipindi wakiingia kwenye eneo la tatu la mwisho la Simba.
Mchezaji mpya wa Yanga, Shekhan Ibrahim Hamis ambaye alisajiliwa kwenye dirisha hili dogo akitokea JKU alionekana kulimiliki zaidi Eneo la Kiungo akishirikiana na Mohamed Omary na Ramadhan Hemedi Ramadhan na kuifanya Simba kupoteana kabisa eneo hili.
Dakika ya 24, Shekhan Hamis alitengewa mpira vizuri na Willyson Christopher kwenye pigo la faulo na yeye kuachia shuti kali akiwa mbali kabisa na eneo la goli na mpira kutinga wavuni, akiwaonjesha tu wana Yanga juu ya ubora wake. 2-0 Yanga.
Dakika ziliyoyoma huku Simba wakishindwa kurejea mchezoni, wakipoteza sana mipira na kushindwa kujenga mashambulizi ya maana. Na hata nafasi walizofanikiwa kuzitengeneza hawakuweza kuzitumia ipasavyo. Pengine magoli mawili ya haraka haraka yaliwatoa mchezoni. Huku Yanga wakizidi kujiamini.
Simba walijaribu kutaka kuuchukua mchezo kati ya dakika 30-40 lakini Dakika ya 45+ Mlinda mlango wa Simba Isihaka alimmfanyia madhambi Ramadhan Hemed na muamuzi kuamuru mkwaju wa penati upigwe ambao nao ulipigwa kiustadi na Ahmed Denis Fredrick na kuiandikia timu yake bao la 3. Mapumziko Simba 0-3 Yanga.
Kipindi cha pili kilirejea huku Yanga wakiendelea kuwasakama wapinzani wao langoni mwao. Simba walikuwa na mapigo mengi golini lakini ni 1 tu ndio lililolenga lango. Bado palikosekana utulivu hasa eneo la mwisho la umaliziaji.
Kiuhalisia ilionekana wachezaji wengi wa Simba kukosa uzoefu. Wakiwa na wachezaji wengi wapya ambao pia wakiwa hawajaweza kutengeneza kuzoeana kuliwafanya waonekana timu ya pili kiwanjani.
Yanga hawakujali hilo, waliendelea kuwaadhibu na dakika ya 60 ya mchezo, Ramadhan Hemed alipokea pasi nzuri kutoka wa Willyson Christopher ambaye amekuwa kwenye kiwango bora sana hii leo, akageuka vizuri na kuachia shuti kali lilimshinda mlinda lango Isihaka Khalfan na kuiandikia Yanga bao la 4.
Wakati Simba wakiendelea kufanya “utoto” zaidi, Yanga walizidisha “Ukubwa”, ukomavu, kujituma na kupanga vema mipango yao. Wakiendelea kuwamiliki Simba watakavyo.
Pengine Yanga wangeweza kuwafunga magoli zaidi Simba kama wangeamua kutengeneza nafasi zaidi lakini walichagua kumiliki mpira na kucheza. Simba walikuwa kwenye mateso haswa ni kama walitamani mechi iishe mapema. Hawakuwa na mkakati wowote na wapinzani wao walikuwa bora kuliko wao kwa mbali sana.
Dakika zote 90 zikatamatika kwa kipyenga cha Kelvin Richard kuashiria alama 3 zinakqenda kwa wageni wa mchezo huu kwa ushindi wa mabao 4-0.