Manchester United wametangaza leo kuwa wameingia makubaliano na Mwenyekiti wa Kampuni ya INEOS, Muingereza Sir Jim Ratcliffe kununua 25% ya hisa za klabu Daraja B na hadi 25% ya hisa daraja A.
Sir Ratcliffe ameshinda mbio hizo baada ya muda mrefu wa mvutano wa kimaslahi na sasa yeye na kampuni yake wanaenda kuwa wasimamizi wakuu wa shughuli zote za kimichezo ndani ya klabu hiyo maarufu duniani.
Pamoja na mambo mengine Sir Ratcliffe pia atatoa hadi $300 Milioni kwa ajili ya uwekezaji wa baadae ndani ya klabu ikiwemo kusimamia Mambo mbalimbali ya kimaendeleo.
Akiongea baada ya makubaliano hayo, Sir Ratcliffe alisema:
Niko hapa Man United kwa ajili ya lengo moja tu la pamoja nalo ni kuirudisha timu pale inapostahili kuwa kwenye ramani ya soka, Uingereza, Ulaya na duniani kote. Nikiwa kama mpenzi wa timu hii maisha yangu yote tangu nikiwa kijana mdogo, nina furaha sana kuweza kuisaidia timu hii kuendesha taratibu zake zote za kimichezo.
Aidha hakusita kuendelea kuwapa moyo mashabiki wa United juu ya kile ambacho wanadhamiria kufanya kwa kipindi watakapochukua Majukumu ya kuiendesha klabu.
Klabu inaingiza mapato mengi lakini hayajatumiwa ipasavyo, tunakuja kuufungua huo mlango. Tunaleta wataalamu wa kazi wenye uwezo mkubwa wa kusimamia maendeleo ya hii klabu kubwa yanasimamiwa ipasavyo kwa sasa na kwa vizazi vijavyo kwakuwa tuko hapa muda mrefu. Tunatarajia mtatuunga mkono maana sisi tupo tayari kushirikiana na kila mtu ndani ya klabu ili kufanikisha kuipeleka mbele klabu yetu.
Pengine hii inaweza kuwa taarifa njema kwa wapenzi wa Manchester United ambao wamekuwa hawaridhishwi na muenendo wa timu yao hivi karibuni. Wengi wakiamini kuwa ukosefu wa bajeti za maana kwenye sajili na miundombinu mingine imechangia kwa kiasi kikubwa kutokana na Glazers kuelemewa. Hata hivyo hii haimaanisho kuwa Glazers wanaondoka tayari.