Connect with us

Makala Nyingine

MECKY : KUTOKA KAGERA NA MATUMAINI KIBAO YA WANA “MBOGO MAJI”

Klabu ya Soka ya Ihefu inayoshiriki Ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara ilimtambulisha Mwalimu Mecky Mexime hapo jana kuwa Kocha wao mkuu mpya akichukua Mikoba ya Kocha Mkenya, Moses Basena ambaye yamepita takribani majuma matatu tangu apewe THANK YOU na wana mbogomaji hao.

Mecky anaichukua Ihefu ikiwa na yeye ametoka kupewa THANK YOU kutoka kwa wana Super Nkurukumbi, Kagera Sugar, siku 5 tu zilizopita. Je Mecky ni chaguo sahihi kwa Ihefu?

Ihefu sio kwamba wamekuwa na timu mbovu msimu huu, na hawakuanza ligi vibaya pia lakini katikati ya safari yakatokea mengi ikiwemo kubadilisha sana makocha, alikuwepo Zubery Katwila kabla ya Moses Basena na wote walikuwa na falsafa tofauti ambazo mara nyingi huwachanganya wachezaji na huchukua muda wakati mwingine mchezaji kuhama na falsafa moja kuhamia nyingine.

Tatizo jingine kubwa lililoikumba Ihefu ni ukwasi wa Majeruhi. Wachezaji wengi hasa wale vinara wa Timu, kama Victor Akpan, Raphael Daud Loth, Juma Nyosso, Joseph Mahundi, Charles Ilanfya na wengineo walikuwa wakipishana kwenye milango ya Daktari. Hili jambo Basena aliwahi kulisema pia. Isingekuwa rahisi timu kurejea kwenye muunganiko wake kiuharaka hivyo kwakuwa pia sio kila mchezaji na ubora wake asilimia 100 kama alivyokuwa kabla ya majeraha.

Hata hivyo huwezi kuwalaumu Ihefu kwa Basena, tangu ameichukua Ihefu hajafanikiwa kuipa hata ushindi mmoja(1). Alianza kwa Suluhu ya 0-0 dhidi ya Coastal Union kabla ya Kupokea Kichapo cha 2-1 kutoka kwa Simba. Sare ya 2-2 dhidi ya Singida FG ilifuatiwa na Kichapo kingine cha 1-3 kutoka kwa Azam FC, kabla ya Kichapo cha 2-0 kutoka kwa Namungo na mechi iliyomuondoa Kikosini ni suluhu ya 0-0 dhidi ya Tanzania Prisons. Akiambulia alama 3 tu kwenye michezo 6. Yani alama alama 3 kati ya 18 zinaowezekana. Ihefu wasingeweza kuvumilia zaidi kutokana na uwekezaji wao.

Themi Felix aliipokea timu kwa Muda ikiwa pia wachezaji wengi wamerejea kutoka majeruhi na wako tayari kutumika. Magoli mawili ya Vedastus Mwihambi yalitosha kuipa ushindi Ihefu wa 2-1 dhidi ya timu ngumu ya Nyuki wa Tabora, Tabora United. Ushindi huo ulifuatiwa na ushindi mwingine dhidi ya ROSPA FC kwenye mashindano ya ASFC wakiinyuka 2-0.

Ikionekana pengine ni ufunuo mpya wa Ihefu chini ya Kocha wa muda Themi Felix, Kipigo cha 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma uliwafanya warudi tena mezani chini ya CEO Biko Skanda kupekua mafaili ya makocha walioomba nafasi na kuliona faili la Mecky Mexime lina CV iliyoshiba wanayoihitaji.

Mecky sio kocha mbaya hata kidogo na ni Mwalimu mwenye historia kubwa na Soka la nchi hii akiwa tayari kafundisha timu nyingi nchini. Akiwa ametoka kufungashiwa virago Kagera Sugar kutokana na mwenendo mbaya wa kimatokeo wa timu hiyo, Ihefu wameiona Lulu na wamepita nayo.

Matumaini makubwa ya wana Mbarali yapo mikononi mwa Nahodha huyu wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania. Wameamini kwenye uwezo wake na uzoefu wake na kuwa kwa wachezaji waliokuwa nao basi hawajachelewa kurudi kwenye malengo yao wakiwa na mtu sahihi.

Hivi karibuni Kagera chini Mecky haijawa na muendelezo mzuri wa matokeo. Tangu washinde 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons wameenda mechi 4 bila ushindi, wakitoka sare 1-1 na KMC kabla ya kufungwa mechi 3 mfululizo, 1-0 dhidi ya Coastal Union, 3-0 dhidi ya Simba na kipigo cha 4-0 nyumbani dhidi ya Azam FC. Kagera hawakuweza kumvumilia kwakuwa timu ina hali mbaya huku ikionekana tatizo sio wachezaji kwani wana vipaji lukuki kama Anuary Jabir, Cleophace Mkandala, Hijjah Shamte, Datius Peter, Dickson Mhilu, Naushad na wengineo.

Mecky anatoka timu iliyo nafasi ya 14 na alama 13 na kuhamia timu iliyo nafasi ya 13 na alama 13. Zote hazipo kwenye nafasi nzuri. Isipokuwa kila mmoja anaamini maradhi yake yanaweza kutibiwa na daktari aliyeshindwa kutibu maradhi ya mwengine. Ni Soka Tu na Imani Zake.

Makala Nyingine

More in Makala Nyingine