Connect with us

Mapinduzi Cup

AZAM WAWAFUNDISHA CHIPUKIZI

Klabu ya soka ya Azam imefanikiwa kupata ushindi wake wa kwanza kwenye michuano ya Mapinduzi baada ya kuwafunga Chipukizi kutoka visiwani Pemba kwa bao 1-0.

Azam FC walipata bao la kwanza dakika ya 12 kupitia kwa Alassane Diao baada ya kugongeana vizuri na Ayoub Lyanga na kupiga shuti la chini chini lililomshinda golikipa wa Chipukizi.

Uwepo wa Kipre Jr leo kwa Azam pamekuwa na faida kubwa sana hasa kwa kuongezeka kasi zaidi kwenye eneo la ushambuliaji. Akitokea upande wa kushoto, Kulia akitokea Lyanga huku Dube akicheza nyuma ya Diao kwenye umbo la 4-2-3-1. Bangala na Akaminko wakicheza nyuma yao.

Dakika ya 20, Ayoub Lyanga alikosa nafasi ya kuipatia Azam bao la pili baada ya kupokea pasi sukari kutoka kwa Yannick Bangala lakini shuti lake lilipaa kidogo juu ya lango.

Chipukizi walishindwa kabisa kuihimili Azam wakizidiwa kila kitu mchezoni. Azam wakionyesha ukubwa wao.

Nathaniel Chilambo alipata nafasi ya kutengeneza bao lakini maamuzi yake ya kuamua kupiga mwenyewe, hayakuwa na faida kwa timu yake.

Azam wangeweza kuongoza kwa magoli mengi kwa namna Chipukizi walivyokuwa wazi lakini ukosefu wa utulivu na maamuzi sahihi yaliwakwamisha. Pengine ni namna Chipukizi walivyokuwa wanawalazimisha Azam kucheza mpira wao wa kupooza. Azam walipooza pia mashambulizi.

Mapumziko Azam FC walitoka kifua mbele wakiwa na utangulizi wa bao 1-0.

Azam walirudi kipindi cha pili wakikianza taratibu huku Chipukizi wakionekana walahu kuchangamka dakika za mwanzo kipindi cha pili wakijaribu kujenga mashambulizi tofauti na kipindi cha kwanza licha ya kwamba bado hawakuwa bora.

Hata kasi ya mchezo haikuwa kubwa kwa timu zote mbili kadri muda ulivyozidi kwenda pakiwa na ufinyu wa nafasi pia. Hakuna shuti lililolenga lango kwa timu zote mpaka dakika ya 70 ya mchezo.

Azam walimtambulisha mshambuliaji wao mpya Franklin Navarro akichukua nafasi ya Kipre Jr. Huku Iddy Selemani Nado akichukua nafasi ya Prince Dube dakika ya 74.

Haikumchukua muda mrefu sana Navarro kujitambulisha japo mashuti yake mawili yote yaliishia kwenye mikono ya golikipa wa Chipukizi.

Azam FC walifanikiwa kuushikilia uongozi wao mpaka dakika ya 90 ya mchezo licha ya kutokuwa na kipindi cha pili bora sana. Alama 3 muhimu baada ya suluhu kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Mlandege.

Alassane Diao wa Azam alichaguliwa kuwa mchezaji Bora wa Mechi.

Makala Nyingine

More in Mapinduzi Cup