Mechi nzuri ikiyotawaliwa na wachezaji wengi vijana. Kipindi cha kwanza kilianza na ufundi mwingi sana huku kila timu ikijitahidi kumiliki mpira na kujenga mashambulizi taratibu.
Mlandege leo walianza na badiliko moja tu kutoka kwenye kikosi kilichocheza dhidi ya Azam FC akianza kwenye benchi leo Jamal Fadhili na kuanza Diego Fernando huku Raphael Futakamba ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Aboubakar Mwadini aliyeumia mchezo uliopita akianza pia leo lakini mfumo ukiwa ule ule 4-3-3.
Wenyeji na mabingwa watetezi walitangulia kupata bao dakika ya 44 ya mchezo dakika 1 tu kabla ya kwenda mapumziko kupitia kwa Optatus Lupekenya.
Vital’O walirejea kwa kasi kipindi cha pili huku wakiwalizimisha Mlandege kucheza nyuma, uwezo mkubwa ukionyeshwa na Nahodha Freddie Niyonizoe kwenye eneo la kiungo akiwapoteza kabisa akina Muhsin Mustafa.
Dakika ya 65, juhudi za Vital’O zikawalipa baada ya kupata bao la kusawazisha kupitia kwa Kessy Nimubona aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu kubwa uliopigwa na Freddie Niyonizoe. 1-1 dakika ya 65.
Mechi iliendelea kunoga huku kila timu ikitafuta bao la ushindi. Timu zote zikifanya mabadiliko kwenye maeneo muhimu yaliyohitaji mabadiliko.
Vital’O walionyesha kuwa hai zaidi hasa dakika za mwisho. Kuingia kwa Jean Nzeyimana ambaye ndie Nahodha hasa wa timu, kulipachangamsha zaidi safu ya ushambuliaji. Lakini walinzi wa Mlandege walikuwa imara.
Dakika zote za mchezo zikatamatika kwa timu zote kupata alama 1 baada ya mchezo kumalizika kwa sare ya 1-1.
Mlandege wanakuwa na alama 2 baada ya mechi 2 sawa na Vital’O.
Abdallah Kulandana aliteuliwa kuwa Mchezaji Bora wa mchezo huku Freddy Niyonizoe akichaguliwa kuwa mchezaji mwenye Nidhamu wa mchezo huu. Hii ni mara ya pili mtawaliwa Freddy anachakua tuzo hii.