Timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” kwa mara ya kwanza imeanza mazoezi yake ya kujiweka sawa katika viwanja vya mazoezi vilivyopo karibu na uwanja mkubwa wa Cairo International kuelekea fainali za mataifa ya Afrika AFCON 2023 zinazotazamiwa kuanza kurindima mapema mwezi huu. Taifa Stars imekita kambi katika mji wa Cairo na inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Misri kabla ya kuianza safari ya kuelekea nchini Ivory Coast.
Afisa habari na mawasiliano wa shirikisho la soka nchini “TFF” ameweka wazi kuwa nyota kadhaa ambao walikuwa hawajajumuika wameanza kujiunga na kikosi hicho, Ndimbo amesema kikosi hicho kitaweka kambi hadi Januari 8 ndipo kitaondoka kuelekea nchini Ivory Coast.
Tumepokea wachezaji wawili leo, Himid Mao Mkami ambaye yeye anacheza hapa Misri, lakini pia tumempokea Khleffin Hamdoun na wote tayari wameanza maandalizi pamoja na wengine.
Ni maandalizi ambayo yatatuweka hapa Cairo Misri mpaka Januari 8, na maada ya hapo kikosi kitafanya safari ya kuelekea pale Ivory Coast kwenye mashindano ya AFCON 2023.
Cliford Mario Ndimbo, Afisa habari na mawasiliano wa shirikisho la soka nchini [TFF].
Baada ya kujiunga na kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” Himid Mao Mkami amewataka watanzania kuwa pamoja na timu kwa kuipa nguvu timu hiyo na wanaamini wanaweza kufanya makubwa kama wakipewa nguvu na watanzania.
Sisi wachezaji na timu tunawahitaji watanzania wenzetu, tunahitaji sana nguvu [saport] yao, nafikiri umoja wetu ndio kitu mhimu sana,… tunaweza kufanya kitu kikubwa zaidi tukiwa wamoja.
Himid Mao Mkami, Mchezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania.
Kocha msaidizi wa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania Hemed Suleiman ‘Morocco’ amesema wachezaji wote waliopo kwenye kambi nchini Misri wapo kwenye Afya njema.
Wachezaji wote ambao wapo kwa wakati huu, wapo kwenye afya njema, siku ya kwanza ya mazoezi imekuwa ni siku nzuri kwetu, tuna zaidi ya wachezaji 20 hapa, … tumejaribu kuamsha mwili tu, ni kitu cha faraja kila mmoja anajaribu kufata maelekezo ili kufanya vizuri.
Hemed Morocco, Kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania.
Timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” ipo kundi “F” na inatarajia kutupa karata yake ya kwanza kwenye fainali za mataifa ya Afrika nchini Ivory Coast dhidi ya Morocco mnamo January 17, Stars ipo pamoja na timu za Taifa za Zambia, Morocco na DR Congo.
Mashindano ya AFCON 2023 yanatarajiwa kuanza kurindima rasmi January 13, mwaka huu, huku Tanzania ikipigiwa chapuo kubwa la kufanya vizuri na wadau mbalimbali kuliko misimu mingine miwili iliyopita ambayo timu hiyo ilishiriki.