DAKIKA 90, Leo zitaamua nani mbabe katika Derby ya Kariakoo kati ya Simba Queens dhidi ya Yanga Princess kwenye mchezo wa mzunguko wa tatu wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania.
Simba Queens watakuwa wenyeji wa mchezo huo, wakiwakaribisha Yanga Princess katika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam, mchezo utakaopigwa majira ya saa 10:00 Alasiri.
Itakumbukwa Kwa msimu huu timu hizo zitakutana kwa mara ya pili, baadavya kukutana kwenye mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii ambapo Simba Queens walifanikiwa kwenda fainali kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya dakika 90 kukamilika kwa sare ya bao 1-1, Goli la Chioma Wogu dakika ya 45+1, likisawazishwa dakika ya 59 na Viviane Aquino Corazone.
Timu zote mbili tayari zimecheza mechi mbili kila mmoja na wote wamefanikiwa kukusanya alama sita[6] katika michezo hiyo ya Ligi kuu ya Wanawake.
Kila timu ipo imara katika safu yake ya ushambuliaji, Simba Queens katika michezo miwili ya Ligi hiyo jumla amefunga mabao 10 na kuruhusu mabao 2 wakati Yanga Princess walitikisha nyavu mara 8 na kuruhusu bao 1, wakipishana kwa goli 1 tu kwenye uwiano wa magoli ya kufunga na kufungwa.
Kuelekea mchezo huo Kocha Msaidizi wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amesema ni mechi ngumu na yenye ushindani mkubwa kwa sababu timu zote mbili zinahitaji pointi tatu kila mmoja kufikia malengo yake.
Amesema wachezaji wake wako tayari kwa ajili ya kupambania timu ili kutafuta ushindi dhidi ya Yanga Princess ambayo iko imara katika kila nafasi.
Tunahitaji kurejesha heshima yetu, ili kufikia malengo hayo lazima tupambane tushinde, tunawaheshimu Yanga Princess ambao wako vizuri lakini kikubwa tunahitaji pointi tatu muhimu. Tutafanya mabadiliko makubwa ya kikosi ambacho kilicheza mechi ya kwanza ya Ngao ya Jamii, tunaingia kivingine na tumejipanga vizuri kwa msimu huu kufikia malengo yetu.
Kikubwa tunatafuta alama tatu iwe idadi ya mabao yeyote yale, wakiingia kwenye mfumo basi tutaweza kufunga idadi ya mabao mengi zaidi, mechi itakuwa nzuri na ufundi ndani ya uwanja.
Kwa Upande wa Yanga Princess, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Charles Haalubono amesema wamejiandaa na ana imani utakuwa mchezo mzuri na wanahitaji matokeo mazuri mbele ya Simba Queens.
Amesema kila mechi lazima iwe na presha hata unapocheza na timu ndogo wanaweza kukupa mechi mgumu kikubwa ni jinsi ya maandalizi ambayo wamejiandaa.
Hatuna majeraha na mashabiki wajitokeze kusapoti itakuwa mechi nzuri na ushindani kwa sababu ya kila mmoja kuhitaji matokeo mazuri ya alama tatu muhimu.