Timu ya Taifa ya Tanzania inaendelea kujifua nchini Misri ilipoweka kambi kwaajili ya fainali za mataifa ya Africa [AFCON 2023] zinazotarajiwa kufanyika nchini Ivory Coast kuanzia January 13 mwaka huu.
Takribani nyota wote walioitwa kwenye kikosi hicho wamewasili kambini na kundi la mwisho likiongozwa na nahodha Mbwana Ally Samatta limewasili jana na tayari wameanza mazoezi ya pamoja.
Nyota wa klabu Shakhtar Donetsk Novatus Dismas Miroshi amesema kila mmoja anajiandaa vyema kwaajili ya mashindano hayo makubwa Barani Afrika ikiwa pia hii ni mara ya tatu [3] kwa Tanzania kushiriki michuano hii.
“Nafikiri kila Mtanzania, kila mchezaji anajua umuhimu wa mashindano, umuhimu wa mashindano ulianzia baada ya mechi na Algeria”.
“Kila mtu anajua majukumu yake, tutaanzia pale tulipoishia mechi na Algeria, ukizingatia tumekuwa na mabadiliko makubwa kwenye timu yetu nafikiri hiyo ndio chachu ya kufanya vizuri katika mashindano”.
Kwa upande wa nahodha wa kikosi cha Yanga, Bakari Nondo Mwamnyeto ameweka wazi ugumu wa kundi ambalo Stars ipo.
“Kundi ni gumu maana timu zote tutakazo kutana nazo ni timu nzuri, na sisi tuna timu nzuri pia”.
“Wachezaji wote wana malengo na mashindano haya na Watanzania watuombee Mungu tu, na sisi pia tupo kupambania nchi yetu kwa asilimia mia kwenye mashindano yanayofuata”.
Timu ya Taifa ya Tanzania itakuwa na kibarua cha kujipima nguvu dhidi ya Misri siku ya Jumapili saa moja [19:00] jioni kabla ya kuianza safari siku ya jumatatu ya kuelekea nchini Ivory Coast.
Bakari Mwamnyeto pia ameielezea mechi hiyo kuwa haitakuwa rahisi na itakuwa kipimo kizuri kuelekea fainali za mataifa ya Afrika nchini Ivory Coast.
“Mchezo huu ni kipimo kwetu, na kipimo kwao pia kwasababu wanaenda katika haya mashindano”.
Tanzania ipo kundi moja na timu ya Taifa ya Congo DR, Zambia na Morocco ambazo zote pia zitacheza michezo ya kirafiki kabla ya kuelekea nchini Ivory Coast.