Aliyekuwa mchezaji wa Coastal Unio Fran Golubic amesema kuondoka kwake katika klabu hiyo kumesababishwa na kushindwa kucheza mechi rasmi hata moja kufuatia klabu hiyo kushindwa kukamilisha baadhi ya taratibu muhimu.
Golubic amesema mara tu baada ya kujiunga na Coastal Union alihakikishiwa taratibu zote za vibali vya kazi na makazi zitakamilishwa haraka ili aweze kucheza lakini badala yake tangu amesaini mkataba mwezi August hadi Disemba 2023 klabu ilishindwa kukamilisha zoezi hilo.
Kila alipowauliza viongozi mchakato umefikia hatua gani aliambiwa zoezi litakamilika ndani ya muda mfupi hivyo ataanza kucheza. Baadae akagundua alikuwa akiambiwa uongo na hakuna mtu yeyote ambaye alikuwa akishughulika na jambo hilo.
“Tatizo hilo halikuwa kwangu peke yangu, wachezaji wenzangu wengine wanne wa kigeni ambao wote tulisajiliwa pamoja kwenye dirisha kubwa lililopita walikuwa na changamoto hiyo hiyo na wote wameondoka kipindi hiki cha dirisha dogo.”
Golubic anasema, kabla ya kujiunga na Coastal Union aliahidiwa kuwa nafasi yake kwenye timu ipo wazi na anasubiriwa yeye tu kitu ambacho kilimfanya ahamasike kujiunga na timu hiyo.
“Baada ya kujiunga na timu nilikuwa nafanya mazoezi kwa bidii ili kumshawishi kocha anipe nafasi ya kucheza lakini mwisho wa siku sijapata nafasi ya kuonesha kile nilichonacho kwenye Ligi ya Tanzania.”
“Kuna mtu mmoja alinieleza ukweli kwamba, klabu ina matatizo ya kiuchumi kiasi kwamba inashindwa kulipa vibali vya kazi na makazi kwa wachezaji wa kigeni.”
Baada ya kukaa Coastal Union kwa miezi mitano [Agosti hadi Disemba] akiishia kufanya tu mazoezi bila kucheza mechi, Golubic aliomba kuvunja mkataba na Wagosi wa Kaya.
Kwa sasa yupo nchini kwao [Croatia] anaendelea na program za mazoezi huku akiendelea kusikilizia ofa nyingine. Kama kuna timu ya Tanzania itakuwa tayari kumsajili, kwa upande wake anasema milango ipo wazi.