Connect with us

Mapinduzi Cup

SIMBA YATINGA NUSU FAINALI, KUIVAA SINGIDA FG

Goli pekee la Jean Othos Baleke, lilitosha kuipa Simba ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Jamhuri na kufanikiwa kutinga hatua ya Nusu Fainali ya mashindano ya Mapinduzi Cup.

Simba walipata nafasi ya mapema kabisa, pigo la Israel Mwenda lilimmfikia Kennedy Juma aliyeurudisha ndani mpira kwa kichwa uliomkuta Fabrice Ngoma aliyepiga shuti lakini golikipa Nasir Talib alikuwa sambamba na shuti hilo.

Jamhuri waliendelea kupata joto la mashambulizi ya Simba waliouanza mchezo kwa kasi sana. Dakika ya 8, Baleke alipata nafasi akipenyezewa pasi na Essomba Onana lakini mpira wake ulidakwa kirahisi na golikipa Nasir.

Mpango mzuri wa kiulinzi waliokuwa nao Jamhuri ulionekana kufanya kazi mpaka dakika ya 25 wakiwa hawajaruhusu bao lakini wakihakikisha Simba hawafanyi sana mashambulizi ya hatari chini ya uangalizi mzuri wa Ikram Bakari na Salum Abdallah.

Luis Miquissone alipiga shuti la mbali nje ya eneo la hatari la Jamhuri lakini shuti lake lilidakwa na golikipa.

Dakika ya 40, Saido Ntibazonkiza alipiga mpira wa faulo ambao hata hivyo haukuwa na madhara kwa Jamhuri, ukimuongezea tu mazoezi Nasir Talib.

Jamhuri waliendelea kuwakera Simba, wakijizatiti haswa kiulinzi. Kila mara Simba wakiamini watapata bao dakika hii, waliwakuta Wapinzani wao wako Imara.

Kunako dakika za 3 nyongeza kabla ya kwenda mapumziko, Jean Baleke aliwainua mashabiki wa Simba baada ya kukwamisha kimiani kwa kichwa krosi maridadi kutoka kwa Luis Miquissone kutokea upande wa kulia.

Mapumziko Simba wanatoka wakiwa kifua mbele kwa bao 1-0.

Shaaban Iddy Chilunda aliingia upande wa Simba kipindi cha pili akichukua nafasi ya Hamisi Abdallah.

Luis Miquissone alimtengenezea nafasi nzuri ya kufunga Shaaban Iddy Chilunda lakini alikosa umakini na kupoteza nafasi hiyo. Dakika ya 55 bado ubao ulisoma 1-0 kwa Simba.

Jamhuri bado waliendelea na nidhamu yao ile ile ya kiulinzi, mara hii wakifika mara chache sana langoni kwa Simba. Ayoub Lakred ni kama alikuwa likizo.

Dakika ya 71 Mchezaji mpya wa Simba, Msenegali Babacar Saŕr alitambulishwa mchezoni sambamba na Salehe Karabaka pamoja na Moses Phiri wakichukua nafasi za Jean Baleke, Luis Miquissone na Saido Ntibazonkiza.

Bado Simba waliendelea kulisakama lango la Jamhuri sana sana wakitumia mapana ya kiwanja.

Mabeki wa Simba walijichanganya na kujikuta wanampa nafasi Mshambuliaji wa Jamhuri kupiga shuti akiwa ndani ya eneo la penati lakini Ayoub Lakred aliiweka salama timu yake kwa kuokoa shuti hilo. Simba waliamshwa hapa dakika ya 85 ya mchezo.

Mechi ilionekana kubadilka dakika hizi za mwishoni, Jamhuri ikiwalazimu kutoka nyuma kutafuta nafasi za kusawazisha goli huku Simba nao bado wakiiona nafasi ya kupata bao lingine lakini pia wakiamua kukaa na mpira ilipobidi kulinda uongozi wao.

Simba walifanikiwa kwenye mpango wao wakiamua kukaa na mpira kusindikiza dakika zilizobakia mpaka dakika zote 90 zilipotamatika.

Mchezo ulimalizika kwa Simba kupata ushindi wa bao 1-0.

Makala Nyingine

More in Mapinduzi Cup