Connect with us

AFCON

WAANDISHI NA PIGO ZA KIMASAI AFCON, WAIPA MATUMAINI STARS.

Timu ya waandishi wa habari ya Tanzania kutoka Clouds fm [Edgar Kibwana, Shaffih Dauda na Mkazuzu] imeelekea nchini Ivory Coast kwa aina yake kwaajili ya kuripoti fainali za mataifa ya Afrika 2023 inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi leo nchini humo.

Tumekuwa tukiziona timu mbalimbali hasa za Afrika magharibi zikiwasili Ivory Coast kwa mavazi ya tamaduni zao sasa imekuwa zamu ya kuwashuhudia waandishi wa Tanzania kutoka Clouds Media nao wakiwasili Abidjan kwa style yao ya Kimasai kama sehemu ya tamaduni ya Tanzania.

Waandishi hao watapata nafasi ya kuishuhudia timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” ikishiriki katika fainali hizi ikiwa ni mara ya tatu kwa timu hiyo kufanya hivyo.

Yahya Mohamed [Mkazuzu] ameeleza kuwa kwa aina ya kundi la Taifa Stars [kundi F] lilivyo kwasasa anaamini kuwa Stars ipo kwenye kundi gumu zaidi na ikitokea timu hiyo imefuzu hatua inayofuata itakuwa ni “Suprise”.

“Wengi tunaamini stars kufuzu tu kwa fainali hizi ni ushindi tosha na kama tutafanikiwa kusonga mbele kwenye kundi letu basi itakuwa kama bonus kutokana na aina ya wapinzani wetu kwenye kundi”.

“Timu tulizonazo kundi F zote zimetuzidi uwezo na uzoefu kwa hiyo chochote tutakachokipata kwetu tunaamin kitatutosha na hatutegemei makubwa, tukivuta hatua ya makundi kwetu na kwenye mashindano itakuwa kitu cha kushangaza [suprise]”, Mkazuzu alisema.

Edgar Kibwana mwandishi wa habari za michezo kutoka Clouds FM ameweka wazi kuwa tutegemee kuona utofauti kwenye mashindano haya na yaliyopita kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa kwe soka kuanzia ngazi ya vijana.

“Ushindani umeongezeka sana, sio tu kwenye swala la zawadi lakini pia kwenye eneo la ufundi, timu nyingi zimefanya uwekezaji mkubwa sana kwenye soka la vijana na miundo mbinu”.

“Nchi ambazo zilikuwa hazijawa na maendeleo makubwa ya soka nazo zimefanya mabadiliko makubwa sana, nchi kama Comoro, Mauritania n.k, kwahiyo tutegemee ushindani mkubwa sana kwenye ushindani”, Ameeleza Edgar Kibwana.

Fainali za mataifa ya Afrika zinatarajiwa kuanza kupigwa rasmi leo kwa mchezo wa ufunguzi kati ya mwenyeji Ivory Coast dhidi ya Guinea Bissau katika uwanja wa Stade Olympique d’Ebimpe.

Mchezo wa ufunguzi utaambatana na shamra shamra kutoka kwa wasanii wakubwa Afrika akiwemo Yemi Alade na zitashuhudiwa na waandishi hawa kutoka Tanzania kwa karibu zaidi na pia wataipa nguvu Taifa Stars katika michezo yake yote mitatu.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Taifa Stars, Mungu wabariki waandishi wetu wote wazalendo waliohudhuria michuano hii.

Makala Nyingine

More in AFCON