Connect with us

AFCON

KIBU KUIONGOZA STARS LEO KUPATA USHINDI WA KWANZA.

Timu ya Taifa ya Tanzania inashuka dimbani hii leo majira ya saa mbili [20:00] usiku kuikabili timu ya Taifa ya Zambia katika mchezo wa pili wa hatua ya makundi ya AFCON 2023.

Tanzania ilipoteza mchezo wa kwanza dhidi ya timu ya Taifa ya Morocco kwa jumla ya goli 3-0 ikiwa chini ya kocha mkuu Adel Amrouche na hivyo matokeo hayo yakaifanya uburuze mkia kwenye kundi F.

Taifa Stars itashuka dimbani hii leo ikiwa chini ya kaimu kocha mkuu Hemed Suleiman Morocco na kocha wake msaidizi Juma Mgunda ambao wote kwa pamoja wamebeba matumaini makubwa kwa Watanzania.

Leo kunatarajiwa kuwepo kwa mabadiliko kadhaa kwenye kikosi cha Stars kutoka kile kilichoanza kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Morocco.

Stars itamkosa Novatus Dismas aliyepata kadi nyekundu kwenye mchezo uliopita huku nafasi yake ikitarajiwa kuchukuliwa na Sospeter Bajana nyota wa klabu ya Azam FC ya Dar Es Salaa.

Kwenye eneo la kushambulia kunatarajiwa kufanyiwa mabadiliko pia huenda leo tukamshuhudia Kibu Denis akiingia kuongeza nguvu akiwa pamoja na Simon Msuva na Mbwana Samatta.

Kwenye eneo la kiungo, nyota wa klabu ya Azam FC Feisal Salum anatajwa kuanza hii leo tofauti na mchezo uliopita ili kuingeza ubunifu kwenye eneo hilo.

Eneo la Ulinzi hakutajwi kuwa na mabadiliko sana licha ya kuwa huenda Dickson Job akachukua nafasi ya nahodha Bakari Mwamnyeto huku eneo la kulia likiendelea kulindwa na Haji Mnoga.

Kocha mkuu Hemed Morocco na Juma Mgunda leo wanazisaka alama tatu mhimu kwenye kikosi chao kwani wakipoteza hii leo basi watakuwa wameyaaga mashindano rasmi na kusubiri kucheza mchezo wa kumalizia hatua ya makundi pekee.

Zambia pia itaingia katika mchezo huu ikiwa na mabadiliko kadhaa kutoka kwa nyota waliocheza kwenye mchezo wa 1-1 dhidi ya DR Congo.

Tanzania haijawahi kupata ushindi wowote kwenye fainali hizi za mataifa ya Afrika tangu imeanza kushiriki, ikitoa sare mara moja [1] na kupoteza mara sita [6] na katika michezo saba [7] iliyopita.

Hivyo inasaka ushindi wake wa kwanza kwenye fainali hizi za mataifa ya Afrika mbele ya Zambia ambayo pia inatafuta ushindi wake wa kwanza kwa takribani miaka 10.

Makala Nyingine

More in AFCON