Klabu ya Simba inafanya mkutano mkuu wa wanachama wake hii leo na inawasilisha ajenda mbalimbali mbele ya wanachama na miongoni mwa Ajenda hizo ni pamoja na mabadiliko ya katiba ya klabu hiyo ya Simba.
Wakati mkutano mkuu huo unaendelea Mwenyekiti wa klabu ya Simba Murtaza Mangungu ameeleza namna ambavyo pesa ya ujenzi wa Uwanja iliyochangwa na wanachama imetumika kujenga ukuta wa kiwanja cha mazoezi cha klabu hiyo huko Bunju.
Aidha Mangungu ameeleza namna ambavyo Klabu ya Simba imenufaika na uwekezaji kutoka kwa wawekezaji mbalimbali waliojitokeza kwenye klabu yao.
“Simba imeshafanya mambo mengi makubwa, yaliyopita, yanayofanyika sasa na mengine yanakuja.”
“Sisi mliotupa dhamana tupo tayari kupokea maoni ambayo yataipeleka Simba mbele.”
“Lengo letu ni kujenga umoja. Mfano mtu anasema uwekezaji hauna faida wakati kabla ya uwekezaji mapato yalikuwa Tsh. 1.6 bilioni, mara baada ya uwekezaji yamepanda hadi Tsh. 6.9 bilioni. Afrika tulikuwa nafasi zaidi ya 80 kwenye ubora na sasa tupo nafasi ya saba. Tunataka ukosoaji wenye tija.”
“Kama mnakumbuka mlichanga pesa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja na pesa ile ilitumika kujenga ukuta wa uwanja wa Bunju na pesa zingine zilitumika kuimarisha kambi ya timu.”
“Tujenge Simba imara kwa kizazi cha sasa na baadae. Tuendelee kushirikiana na naamini Mwenyezi Mungu atatutangulia. Mkutano umefunguliwa.”- Mwenyekiti wa Klabu, Murtaza Mangungu.
Klabu ya Simba ipo kwenye mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo, na mabadiliko hayo yanaanza na marekebisho ya katiba ya klabu hiyo.