Klabu ya Simba imemaliza mchezo wake wa michuano ya ASFC dhidi ya klabu ya Tembo kwa ushindi wa goli 4-0.
Alikuwa Luis Miquissone aliyeitanguliza Simba kwa kuipatia goli la mapema la mchezo mnamo dakika ya 11 na baadae Said Ntibanzokiza akaiandikia goli la pili dakika ya 31 kabla ya mapumziko.
Kipindi cha pili cha mchezo huo kilishuhudia magoli mengine mawili yakiwekwa kimiani na nyota wapya wa kikosi hicho waliotokea benchi.
Dakika ya 81 ya mchezo Saleh Karabaka nyota aliyesajiliwa dirisha la mwezi January akitokea visiwani Zanzibar aliiandikia goli la tatu klabu hiyo akitokea benchi.
Pa Omar Jobe nyota anayetabiriwa makubwa kwenye kikosi hicho alitamatisha karamu ya magoli kwa kuiandikia goli la nne klabu ya Simba dakika ya 83 ya mchezo.
Baada ya mchezo huo kocha wa kikosi cha Tembo inayoshiriki Ligi daraja la tatu amesema kuwa licha ya kupoteza mchezo huu lakini kuna mengi waliyojifunza na wataenda kuyatumia katika michezo ya Ligi daraja la tatu.
“Nashukuru vijana wangu wamecheza vizuri, mechi hii imetuongezea mambo mengi sana kuelekea michezo yetu ya ligi daraja la tatu”, Alisema kocha wa Tembo fc.
Kwa upande wa Seleman Matola kocha msaidizi wa kikosi cha Simba amesema kuwa mechi hii imewapa taswira nzuri kuelekea michezo yao inayofuata.
“Mechi hii imetupa taswira nzuri kuelekea mechi zinazofuata na tumejua nani anacheza wapi”, Amesema Seleman Matola kocha msaidizi wa Simba.
Kwa upande wa viwango vya nyota wao wapya Matola ameeleza kuwa kuna kitu watakiongeza kwenye kikosi chao kutokana na uchangamfu waliouonyesha kwenye mchezo wa leo.
“Ni wachezaji wazuri na wamechangamka, watatusaidia kwenye michezo yetu inayofuata”, Alimaliza Selema Matola.
Baada ya mchezo huo, klabu ya Simba itaianza safari kesho kuelekea mkoani Kigoma ambapo wana mchezo wa Ligi dhidi ya Mashujaa, Jumamosi February 3 kwenye Dimba la Lake Tanganyika.
“Tunatarajia kuondoka kesho kwaajili ya mchezo wetu dhidi ya mashujaa, unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi, kwenye uwanja wa lake Tanganyika”.
Tunaenda kucheza kwenye uwanja mgumu sana nchini Tanzania, lakini tunaamini kwaaina ya maboresho tuliyoyafanya kwenye dirisha dogo la usajili tutaondoka na alama tatu”, Amesema Ahmed Ally, Afisa Habari wa klabu ya Simba.