Raisi wa Shirikisho la Ngumi Tanzania Ndugu Lukelo Willilo, amempongeza Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dr. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuthamini maendeleo ya sekta ya michezo nchini Tanzania.
Willilo aliyasema hayo baada ya kuifikisha timu ya Taifa ya Ngumi katika kambi ya kudumu katika kituo cha Shule ya Filbert Bayi, Kibaha – Pwani kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya Afrika Accra 2023 yatakayofanyika kuanzia tarehe 8-23 March, 2024 katika Jiji la Accra, Ghana.
Mama Samia amekua bega kwa bega na mafaniko yetu katika michezo kutoka kufadhili Timu ya Taifa iliyoshiriki michezo ya Jumuiya ya Madola ya Birmingham 2022 ambapo Tanzania ilipata medali 3 (2 zikiwa za Ngumi) baada ya miaka 16.
Mwaka 2023 Serikali yake iliwezesha Ngumi kushiriki mashindano ya Ubingwa wa Afrika na kufanikiwa kurudi na medali 2 (1 ikiwa ya Fedha ya Mwanamke wa kwanza Tanzania ya Grace Mwakamele) na kushiriki mashindano ya kufuzu Olimpiki kwa Afrika Dakar, Senegal na kurudi na medali ya Fedha ya Yusuf Changalawe.
“Mafanikio ya Harambee ya timu za Taifa yameanza kuonekana, kwa niaba ya wanufaika wote tunazishukuru Taasisi za Serikali na binafsi, na wadau wote walioahidi na kuwezesha harambee ile, na nawasihi ambao bado hawajatekeleza kufanya hivyo kwa maendeleo ya michezo Tanzania” alisema Ndugu Willilo.
Timu hio ilioyoingia kambini ina jumla wa wachezaji 17 (11 wanaume na 6 wanawake) itakuwa chini ya Mwalimu Mkuu Samwel Beatmen Kapungu.
Wakati huohuo, Nahodha wa Timu ya Taifa Yusuf Changalawe anatarajiwa kwenda kambi nje ya nchi kwa kusimamiwa na Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC) kwa ajili ya kujiandaa mashindano ya kufuzu Olimpiki ya Paris 2024 yatakayofanyika tarehe 4-11 March, 2024 Busto Arsizio, Italy.
Baada ya mashindano hayo Changalawe ataungana na wenzake Accra, Ghana katika mashindano ya Afrika.
Pia kambi ya Timu B ya Taifa inaendelea na mazoezi yake katika kituo cha JKT Mgulani.
Pamoja na mchezo wa ngumi, Timu ya Taifa ya Judo pia imeweka kambi katika kituo hichi ikiwa na jumla ya wachezaji na viongozi 16.